• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
ONYANGO: Serikali ilinde hadhi ya wanawake wa vijijini

ONYANGO: Serikali ilinde hadhi ya wanawake wa vijijini

Na LEONARD ONYANGO

WANAWAKE nchini leo wanaungana na wengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake huku kauli ya mwaka huu ikiwa: “Chagua Kushindana”.

Kushindana na vikwazo vinavyotatiza juhudi za kuwepo kwa usawa wa kijinsia.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, mambo yanayoangaziwa ni: kupongeza wanawake ambao wamefana katika teknolojia na ubunifu, usawa wa wanawake katika spoti, kuelimisha wanawake kuhusu maamuzi ya kiafya, kuhakikisha wanawake wanastawi katika sehemu zao za kazi, kuhakikisha kuwa ubunifu wa wanawake unaonekana na kuwasaidia wanawake kujistawisha kiuchumi.

Kati ya mambo hayo sita yanayoangaziwa mwaka huu; kuwasaidia wanawake kujistawisha kiuchumi ingali ni changamoto, haswa katika maeneo ya vijijini.

Wengi wa wanawake katika maeneo ya vijijini wanaishi maisha ya uchochole kwa sababu wanategemea shughuli ambazo zimeathiriwa pakubwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile kilimo, maji, samaki kati ya nyinginezo.

Tafiti zinaonyesha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mafuriko, ukame na mizozo ya rasilimali huathiri wanawake zaidi ikilinganishwa na wanaume.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa 2018 ilionyesha kuwa mapigano yanapotokea kutokana na mizozo ya malisho, maji, asilimia 80 ya wanawake huathirika.

Kulingana na utabiri wa wizara ya Mazingira, mito mingi inatarajiwa kukauka ndani ya miongo mitatu ijayo.

Kulingana na takwimu za wizara, barafu iliyosalia katika kilele cha Mlima Kenya inatarajiwa kuisha ndani ya miaka 30 ijayo.

Kuisha kwa barafu hiyo kutasababisha mito kadhaa ambayo inategemea maji kutoka katika Mlima Kenya kukauka.

Kwa mujibu wa serikali, joto limekuwa likiongezeka kwa kasi nchini tangu miaka ya 1977.

Joto hilo linamaanisha kuwa vyanzo vya maji vitakauka. Uhaba wa maji unapotokea ni wanawake ambao hulazimika kutembea kwa umbali mrefu kutafuta bidhaa hiyo hivyo kupoteza wakati ambao wangetumia katika shughuli za kujitafutia mapato.

Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya chakula kinachotumiwa humu nchini kinazalishwa na wanawake.

Ongezeko la ukame na mvua kubwa inayosababisha mafuriko na kuharibu mazao mashambani ni pigo kwa wanawake wanaojipatia mapato kupitia kilimo.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Muungano wa Mashirika ya Uhifadhi wa Mazingira Duniani (IUCN) na kuchapishwa Januari 20, mwaka jana ilibaini kuwa kuna uhusiano baina ya mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la dhuluma dhidi ya wanawake.

Ripoti hiyo, kwa mfano, ilisema kuwa mabadiliko ya tabianchi yamechangia katika kusababisha kupungua kwa samaki baharini na maziwani hivyo hali hiyo inalazimu wanawake ambao wanategemea biashara ya samaki kujiingiza katika ukahaba.

Tutaendelea kuishi na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa muda mrefu hivyo serikali ya kitaifa na kaunti hazina budi kuhakikisha kuwa miradi inayolenga kuinua kiuchumi wanawake wa vijijini inapewa kipaumbele.

You can share this post!

Bale na Kane waongoza Tottenham kuwateremkia Crystal Palace...

WARUI: Vyuo vikuu vimetapakaa kote si ajabu ubora umeshuka