• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Bale na Kane waongoza Tottenham kuwateremkia Crystal Palace katika EPL

Bale na Kane waongoza Tottenham kuwateremkia Crystal Palace katika EPL

Na MASHIRIKA

GARETH Bale na Harry Kane walifunga mabao mawili kila mmoja na kusaidia kikosi chao cha Tottenham Hotspur kuwapepeta Crystal Palace 4-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumapili usiku.

Ushindi huo ulikuwa wa tatu mfululizo kwa kikosi cha Tottenham kinachonolewa na kocha Jose Mourinho kusajili katika kampeni za ligi muhula huu.

Bale anayewachezea Tottenham kwa mkopo kutoka Real Madrid, alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 25 kabla ya kuongeza na pili mwanzoni mwa kipindi cha pili. Magoli yote mawili yaliyofungwa na fowadi huyo raia wa Wales yalichangiwa na Kane ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza.

Ingawa Christian Benteke aliwasawazishia Palace katika dakika ya 45, bao lake lilichochea ufufuo wa makali ya Tottenham waliofungiwa bao la tatu na Kane katika dakika ya 52 kabla ya kapteni huyo wa kikosi cha Mourinho kupachika wavuni goli jingine katika dakika ya 76.

Bao lililofungwa na Benteke lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Luka Milivojevic. Fowadi raia wa Ivory Coast Wilfried Zaha aliyekuwa akirejea katika kikosi cha kwanza cha Palace baada ya kuweka nje na jeraha la goti, alishuhudia makombora yake mawili yakigonga mhimili wa lango la Tottenham.

Kichapo ambacho Palace ya kocha Roy Hodgson ilipokea kiliwasaza katika nafasi ya 13 kwa alama 34, nane pekee nyuma ya Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Kwa upande wao, Tottenham waliwaruka West Ham United na mabingwa watetezi Liverpool na kupaa hadi nafasi ya sita kwa alama 45, mbili nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora.

Everton ya kocha Carlo Ancelotti itavaana na Chelsea mnamo Machi 8, 2021 uwanjani Stamford Bridge katika mechi inayotarajiwa kuendeleza vita vikali vya kupigania fursa ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora. Everton kwa sasa wanakamata nafasi ya tano kwa pointi 46 japo wana mechi moja zaidi ya kusakata ili kufikia idadi ya michuano 27 ambayo imetandazwa na Chelsea na Tottenham.

MATOKEO YA EPL (Machi 7, 2021):

West Brom 0-0 Newcastle United

Liverpool 0-1 Fulham

Man-City 0-2 Man-United

Tottenham 4-1 Crystal Palace

You can share this post!

Manchester United wapiga Manchester City breki kali ligini

ONYANGO: Serikali ilinde hadhi ya wanawake wa vijijini