• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Orengo amchangamkia Ruto na kumwita ‘Mtukufu Rais’ licha ya uhasama wa kisiasa

Orengo amchangamkia Ruto na kumwita ‘Mtukufu Rais’ licha ya uhasama wa kisiasa

Na LABAAN SHABAAN

Baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 ulioishia Rais William Ruto kuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya, viongozi wa mrengo wa upinzani wa Azimio la Umoja wamekuwa wakidinda kumtambua Dkt Ruto kuwa rais.

Ijapokuwa Dkt Ruto amekuwa akirusha ndoana na kunasa makumi ya wajumbe wa Azimio, wapo wengine ambao wamekaa ngumu kukiri paruwanja yeye ni rais wakiongozwa na kinara wao Raila Odinga.

Rais ameanza ziara ya siku nne eneo la Nyanza na alipofika kaunti ya Siaya, Gavana wa kaunti hiyo James Orengo alimwita ‘mtukufu rais.’

Hotuba ya Bw Orengo iliyomtukuza rais ilipachika furaha na tabasamu nyusoni mwa viongozi wa serikali waliohudhuria wakiwemo wakazi.

Aliposimama kuhutubu kuhusu ziara ya maendeleo Siaya, Bw Orengo alisema, “…tumeelezewa serikali ilikuwa tayari kuweka Sh57 milioni katika kituo hiki cha afya (Ugenya) kiwe level 4 na tumeongea na Waziri wa Afya (Susan Nakhumicha) mtukufu rais…wacha nisema mtukufu rais….tulizoea sana…tumeongea jinsi hii hospitali itajengwa namna gani.”

Bw Orengo alionekana kumkweza Dkt Ruto katika kiwango ambacho awali rais wa pili wa jamhuri ya Kenya marehemu Daniel Moi alikuwa akirejelewa na vyombo vya habari pamoja na viongozi wa serikali.

Gavana wa Siaya alidhihirisha undumakuwili kwani alikuwa mstari wa mbele kupinga viongozi wa upande wa upinzani kama vile Mbunge wa Langata Felix Odiwuor kukutana na baba wa taifa ikuluni na kumtambua kuwa rais.

“Mtu hawezi kuniuliza ninafanya nini hapa kukutana na rais kwa sababu katiba ndiyo imesema ya kwamba serikali ya kitaifa lazima ifanye kazi na ile ya kaunti. Hii siasa ambayo tunafanya, katiba ilimaliza,” Bw Orengo alisema akisherehekewa na wakazi.

Haya yanajiri wakati kamati ya kitaifa ya maridhiano inayohusisha upande wa serikali na upinzani inaendeleza mijadala ya kuleta mwafaka kati ya serikali ya Kenya Kwanza na mrengo wa upinzani Azimio la Umoja.

  • Tags

You can share this post!

Kutana na Mzee Mohamed Mbwana Shee almaarufu ‘Kamusi...

Kisura wa pembeni anataka nigharamie mahitaji eti hana kazi

T L