• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Ruto sasa ashtua watoto wa kuanzia miaka 3 na nauli za treni

Ruto sasa ashtua watoto wa kuanzia miaka 3 na nauli za treni

NA SAMMY WAWERU

SHIRIKA la Reli Nchini limetangaza kutathmini upya ada za usafiri kwa njia ya reli, ambapo sasa watoto watakuwa wakilipiwa nauli.

Kupitia taarifa, shirika hilo limesema watoto walio na umri kati ya miaka 3 hadi 11, watalipa nusu nauli ya ada inayotozwa watu wazima.

Na kwa waliofikisha miaka 11 hadi 17, watakuwa wakilipiwa nauli sawa na watu wazima kuanzia Januari 1, 2024.

“Madaraka Express Passenger Service, mabadiliko ya nauli za treni kuanzia Januari 1, 2024…Watoto walio kati ya miaka 3 – 11 wanaosafiri na watu wazima, kila mmoja atalipiwa nusu nauli ya ada inayotozwa mtu mzima,” linadokeza tangazo hilo, ambalo limeainisha ada za kusafiri maeneo mbalimbali kwa njia ya treni.

Linaendelea kueleza: “Kwa watoto wenye umri zaidi ya miaka 11, watalipa nauli sawa na ya watu wazima. Walio chini ya miaka 3, hawatalipia.”

Huduma za usafiri na uchukuzi kupitia reli na treni za kisasa (SGR), zilizinduliwa Mei 2017 chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Treni ilikuwa ikihudumu – kusafirisha watu wakati wa enzi za Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na mrithi wake, Daniel Arap Moi, wote kwa sasa wakiwa marehemu.

SGR inahudumu kati ya Nairobi, Mombasa na Suswa Naivasha.

Kwa wenye mapato ya chini na ya kadri (economy class), jedwali la SGR linaonyesha nauli kati ya Nairobi na Mombasa imekuwa Sh1, 500.

Na kutokana na tangazo la Shirika la Reli Kenya, ina maana kuwa kila mtoto aliye kati ya miaka 3 – 11 atakuwa akilipa Sh750 kuenda Mombasa, kutoka Nairobi.

Daraja la matajiri (first class), nauli ya Nairobi hadi Mombasa imekuwa Sh4, 500 na hii ina maana kuwa watoto wenye umri wa miaka 3 hadi 11 watakuwa wakilipiwa Sh2, 250.

SGR ilizinduliwa na Bw Kenyatta, japo ilikuwa mradi wa Rais marehemu Mwai Kibaki, ili kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi kati ya Nairobi na Mombasa, na kurejea.

Ujenzi wa mradi huo wa uchukuzi kwa njia ya treni uligharimu karibu nusu trilioni, chini ya ufadhili (mkopo) wa serikali ya Uchina.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Siri ya kumudu Karatasi ya Pili ya KCSE Kiswahili kama...

Mwanamuziki Ali Khamis almaarufu Ally B aaga dunia

T L