• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
Safari ndefu ya mwanachuo kusaka maisha bora baada ya kuugua ukoma

Safari ndefu ya mwanachuo kusaka maisha bora baada ya kuugua ukoma

Na MAUREEN ONGALA

MAKOVU ya vidonda miwilini, kuanzia kwa mikono hadi miguu, ndilo thibitisho pekee kwamba Francis Thoya alikuwa ameugua ugonjwa wa ukoma.

Ngozi yake ni nyororo na laini. Thoya, 29, anatoka kijiji cha Maziyani katika kata ya Ngerenya eneo bunge la Kilifi Kaskazini, Kaunti ya Kilifi. Kila unapokutana naye hakosi tabasamu.

Anasema furaha hiyo ni kumshukuru Mungu kwa kumponya ukoma. Hii ni baada ya kasisi mmoja kwa jina Josiah Kalume, wa Joy Fellowship Ministries mjini Tezo, Kilifi, kumwombea kwa kipindi cha mwezi mmoja mnamo 1991.Anasema mchungaji huyo alikuwa akifanya maombi ya kufunga na aliamka siku moja akapata ukoma umetoweka baada ya kipindi hicho cha mwezi mzima.

Akizungumza na Taifa Leo katika shughuli zake za kila siku za kuuza samaki aina ya papa, Thoya alisimulia jinsi familia yao ilivyotengwa na jamii sababu ya kuwa na mtoto mwenye ukoma.

Anasema kwamba alijua yuko na ugonjwa huo akiwa na miaka tano wakati aliona hakuna mtu alitaka kuwa karibu naye kwa sababu ya harufu.

“Nilijiona tofauti na watoto wengine na hapo ndipo mamangu alinieleza kwamba nilikuwa naugua ugonjwa ambao sio wa kawaida.“Wakati huo sikuelewa kilichokuwa kikiendelea maishani mwangu sababu ya maisha ya upweke. Hakuna jirani wala mtu yeyote wa jamii yetu aliyekuja kututembelea, hivyo tuliishi maisha ya upekwe sana,” anaeleza.

Mahangaiko na changamoto tele ziliwakumba wazazi kutafuta matibabu. Walimpeleka hospitali bila mafanikio; mwishowe wakaanza kutafuta usaidizi wa waganga. Mambo yalizidi kuwa magumu baada ya kifo cha babake wakati Thoya alikuwa na umri wa miaka sita.

Kila kukicha mamake aliendelea kukosa matumaini yake kupona kupitia madaktari hospitalini, na kuzidi kwenda kwa waganga. Kulingana na Thoya, mamake alifanya kila awezalo kumpa mwanawe uponyaji na kuepuka kejeli za familia na jamii. “Baadhi ya wanajamii hata walimwambia mamangu eti sikustahili kushi,” asema kwa huzuni.

Hata hivyo, maombi ya mamake yalijibiwa baada ya mtumishi huyo Pasta Kalume kumwombea na akapata kupona mwaka 1991. Ingawa alikuwa na umri mkubwa wa miaka 11 alianzia darasa la kwanza katika shule ya msingi ya Mrimawandege eneo bunge na Ganze.

Mwaka 2004 alifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) na kupata alama 386. Mamake, ambaye alikuwa akifanya vibarua vijijini ili kuwalea, alikosa karo ya kumplekea Shule ya Upili ya Mangu alikoitwa, hivyo ikamlazimu kujiunga na shule ya wavulana ya Sokoke.

“Maisha yalizidi kuwa magumu kila siku. Mama alishindwa kunilipia karo kwani gharama za kuwatunza watoto sita zilimlemea. Ilibidi wahisani kadha wajitokeze kunisaidia ili nimalize masomo yangu,” anahoji.

Thoya alipata alama ya C+ katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) mwaka 2009 na kama ilivyo ada hakuwa na fedha za kwenda chuo kikuu.Akasaka ajira kama mfanyakazi wa nyumba baada ya matokeo ili kumsaidia mama kulea ndugu zake.

Alikuwa analipwa Sh2,500 kwa mwezi kwa kazi zote za nyumbani alizofanya; ikiwemo kufua, kupiga deki na kupika. “Niliweka kiwango kidogo cha mshahara na nilipokuwa tayari kwenda chuoni nilifanya mchango ili kupata pesa zaidi,” anaendelea kusimulia.

Alijisajili mwaka 2017 katika Chuo Kikuu cha Pwani kusomea Shahada kaatika Masuala ya Jamii.Hii ilikuwa baada ya kukaa nyumbani miaka minane. Hata hivyo, alilazimika kusitisha masomo kama wanafunzi wengine baada ya shughuli za elimu na zingine nchini kusitishwa kufuatia kuzuka kwa janga la corona mnamo Machi 2020.Thoya aliamua kuanza kuuza papa wakati wa likizo hiyo ndefu.

Ni biashara ambayo ameikolea kiasi cha kupewa jina ‘Papa Man’. “Hakuna kazi nyingine ningeweza kufanya wakati huo. Niliamua kuuza samaki ili kupata kipato na pia kulea familia yangu kwani mama sasa amezeeka.

”Hata hivyo, bado anataka kutimiza ndoto yake ya kuwa na elimu bora – msukomo ukiwa nafasi aliyoikosa ya kujiunga na shule ya Mangu sababu ya umaskini.Thoya anaendeleza biashara yake katika vijiji na miji ya Kilifi, na hata ana wateja katika ofisi za kaunti.Kila wiki husafiri hadi Gongoni kununua papa katika soko la samaki.

Biashara hii imekuwa rahisi kwake sababu papa hudumu kwa meizi kadhaa anapopakwa chumvi na kukakushwa kabisa.“Ilikuwa changamoto nilipoanza kwani kila nilipopita njiani watu waliniambia ninanuka papa. Hata baadhi ya weteja wa nyumbani walinikejeli kutokana na harufu hiyo,” asema.

Akiwa mtoto wa sita na kifunga mimba, Thoya aeleza kuwa umaskini uliwafanya wakubwa wake kutofikia na elimu ya juu.“Ndugu zangu walifanikiwa kufika hadi shule ya upili tu. Lakini dada zangu watatu waliolowa baada ya kumaliza darasa la nane.”

Licha ya haya yote aliamua kutumia akiba ya pesa alizokuwa nazo kumjengea mamake nyumba ya kisasa – yenye paa la mabati na ukuta wa mawe na saruji. Japo sio nyumba ya kifahari alikuwa na ndoto ya kumtoa mamake katika nyumba ndogo aliyokuwa akiishi yenye kuta za matope na paa la makuti.

Anaeleza: “Kwa miaka mingi sana mamangu ameishi maisha duni bila hata nyumba. Wakati wa mvua paa lote lilikuwa linavuja na mara mingi alikesha usiku kucha huku matope yakianguka kutoka ukutani.”

Kila mara baada ya mvua kunyesha iliwabidi kununua makuti ya kurekebisha paa hilo, na pia kusaka udongo wa kuziba nyufa ukutani. Thoya anapanga kuandaa hafla kubwa itakayotimiza malengo mawili; kuchangisha pesa zaidi kuongezea akiba aliyonayo ili kulipia karo ya sh160,000.

Vile vile, kuvutia wadau na watalii kupitia jumbe za hamasisho kuhusu bidhaa za ziada zinazotengenezwa kutokana na papa; ikiwemo biskuti ambazo zina virutubishi kwa watoto wachanga wa miaka tano.

Nia yake ni kuwa balozi wa masuala ya uchumi wa rasilimali za baharini – kwa Kimombo Blue Economy. Isitoshe, Thoya analenga kutumia hafla hiyo – anayoita Sherehe ya Papa – katika ufuo wa Ngala Beach mnamo Mei 25, kuwaelimisha vijana wenzake jinsi ya kutumia raslimali zinazopatikana katika maeneo yao ili kujiendeleza maishani na pia kutengeneza nafasi za ajira.

Anafahamu ilivyo changamoto kubwa kwa wanafunzi maskini katika vyuo vikuu kulipa karo yao na hivyo kuishia kusitisha masomo.

“Vijana wengi hawana kazi, wanafunzi wengi chuoni wanaotoka familia zisizojiweza hupitia changamoto kupata karo.“Lakini tukiangalia kwa upande mwingine, kuna nafasi nzuri za kutumia raslimali za baharini kama kitega uchumi,” anaeleza.

You can share this post!

Rais Suluhu aachilia huru wafungwa 5,001

Gavana aliyeachia mke mamlaka ang’olewa uongozini licha...