• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:46 PM
SHINA LA UHAI: Hijama: Utaratibu unaotibu maradhi mbalimbali

SHINA LA UHAI: Hijama: Utaratibu unaotibu maradhi mbalimbali

NA FARHIYA HUSSEIN

MFUMO wa matibabu uitwao hijama (cupping) au kuumika au ukipenda kupiga chuku ambao umekuwa ukitumika tangu jadi sasa umeanza kukubalika na wengi kama njia mbadala ya kutibu maradhi mbalimbali mwilini.

Hijama ni neno la Kiarabu linalomaanisha ‘kutoa’. Tiba hii hutumika kama njia mojawapo ya kusafisha damu mwilini.

Asilimia 80 ya magonjwa hutokana na damu kushindwa kuzunguka vizuri mwilini. Aidha viungo vya mwili hushindwa kufanya kazi vizuri damu inapokuwa imejaa uchafu au sumu ambayo mara nyingi isipoondolewa, huhatarisha zaidi afya ya mwathiriwa.

Aidha hijama imetajika kuwa salama na isiyokuwa na madhara na hutumika sana kuzuia maradhi zaidi mwilini.

Kulingana na Dkt Zubeir Mohammed, mmoja wa wataalamu wanaokumbatia mfumo huu wa matibabu, alichagua aina hii ya tiba baada yake kuugua kiasi cha kutoweza kusimama wala kutembea bila usaidizi. Anasema hata kwenda msalani ilibidi ashikiliwe ili aweze kutembea.

Dkt Zubeir Mohammed akimafanyia mgonjwa tiba ya kupiga chuku yaani hijama. PICHA | WACHIRA MWANGI

Na baada ya kupata nafuu, alikata kauli kufungua kituo kinachojulikana kama Siha Centre, katika Kaunti ya Mombasa ilikuweza kutoa huduma hii.

“Nilikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka miwili. Lakini nilipokumbatia hijama kama mfumo wa matibabu, sikuamini matokeo. Nilipona na ndio sababu kuu iliyonisukuma kufungua Siha Centre,” anasema Dkt Mohammed huku akiongeza kuwa bado hufanyiwa hijama kila mwezi.

Anasema kuwa kwa siku huwa anapokea wagonjwa zaidi ya watano. Lakini pia anasisitiza kwamba hakubali kumhudumia mgonjwa yeyote bila rekodi au stakabadhi muhimu zilizotolewa na daktari baada ya uchunguzi wa maradhi aliyonayo.

“Kabla sijaonana na mgonjwa, hatua ya kwanza ni kumuuliza kama ana tatizo lolote la kiafya au anapendelea hijama ili kuboresha afya tu (Wellness). Ikiwa ni kutokana na maradhi yoyote, basi nitahitaji matokeo ya uchunguzi wote wa kimatibabu, kabla ya kuanza kumfanyia hijama,” anasema.

Tiba hii inajumuisha vikombe maalum al-maarufu hijama cups ambavyo huwekelewa katika sehemu tofauti mwilini, kama vile kichwa, mikono, shingo, mgongo na pia miguu. Hatua hii husababisha tishu zilizo ndani ya kikombe kuvutwa/kunyonywa hivyo kuzidisha mtiririko wa damu katika eneo lililoathirika (suction).

Dkt Mohammed anaeleza kuwa kila ugonjwa una mahala pake maalum pa kuwekelea kile kikombe hicho.

“Kila ugonjwa una sehemu maalum ya kuwekelea vikombe, iwe ni ugonjwa wa kisukari au maumivu ya hedhi. Tunaziita sehemu za kuondoa sumu mwilini,” anasema.

Alianza kwa kuwafanyia familia yake aina hii ya matibabu kabla ya kuelekea nchini Tanzania na kujifunza zaidi.

“Nyanya yangu alikuwa akiwafanyia watu hijama. Lakini enzi hizo walikuwa wakitumia vifuu vya nazi wala si vikombe vya kisasa tunavyotumia sisi,” aeleza.

Kuna aina mbili za matibabu ya hijama, dry na wet cupping. Katika dry cupping hakuna sehemu inayokatwa ila wet cupping, sehemu ilivutwa na kikombe hukatwa kijipande kidogo kwa kutumia wembe kuondoa damu chafu.

“Aina hizi mbili hutegemea na afya ya mtu, ikiwa ni kwa ajili ya kuboresha afya(wellness), tunafanya wet cupping. Lakini ikiwa ni kwa ajili ya kutibu maradhi, basi utaratibu wa njia tofauti hufuatwa, ikiwa ni shughuli ya siku tano,” anaeleza.

Hatua za matibabu

Siku ya kwanza inahusisha kutambua sehemu za kuekelea vile vikombe.

Vikombe vya hijama. PICHA | MAKTABA

Sehemu hizi zinajulikana kama acupressure points.

“Binadamu wana takribani acupressure points 360 ambazo zimeunganishwa na viungo muhimu kama figo na moyo. Kwa hivyo sehemu hizi zinapoathirika, husababisha maumivu na kuvimba. Kumaanisha kuwa mzunguko wa damu mwilini umekatika. Katika hatua hii, tunachofanya ni kufungua mishipa ili mzunguko wa damu uimarike na kupunguza maumivu ya mwili,” anasema.

Siku ya pili itahusisha ukandaji wa sehemu hizo kwa kutumia kikombe kinachofahamika kama soft tissue massage.

“Siku ya tatu tunawekelea vikombe nane kwenye sehemu ya nyuma ya mwili kisha damu inavutwa ndani ya kikombe kuzidisha mtiririko. Hii hutumika sana kwa watoto wadogo na wagonjwa wa upungufu wa damu kwa sababu hawana damu ya kutosha,” anasema.

Katika matibabu ya hijama, rangi ya damu ndiyo hutumika kuelezea jinsi hali ya afya ilivyo.

“Mtu akifanyiwa hijama kisha rangi ya damu yake iwe nyekundu, ina maana ni mzima wa afya. Ikiwa ni nyekundu iliyokolea au hudhurungi, hiyo inamaanisha kuwa mfumo wa mwili ni mbovu na mzunguko wa damu hauko sawa,” aeleza Dkt Mohammed.

Aina ya tatu ni pale damu inapokuwa nyeusi, hii inaashiria kuwa mgonjwa yuko katika hali hatari kiafya. Aidha anaweza akaugua mshtuko wa moyo. Aina hii ya damu pia hutoa harufu mbaya.

Hijama inatumika pia kutibu wanawake wenye maumivu ya hedhi na uvimbe wa fibroids au pia matatizo yanayoaminika kutokana na uchawi.

Gharama ya matibabu

Kwa Sh4,000, unaweza ukapata matibabu ya hijama endapo unaugua maradhi yoyote. Hata hivyo ikiwa unataka kufanyiwa utaratibu huu kuboresha afya tu, basi utagharimika Sh1,500.

Dkt Mohammeda anaeleza kuwa huwatibu watoto kati ya miezi minane na kumi bila malipo ila wazazi watahitajika kununua dawa za mitishamba kutoka kwake.

Tangu kufungua Siha Centre 2016, anasema ameweza kuwashughulikia zaidi ya wagonjwa 3000.

“Watu wanaanza kukumbatia matibabu ya hijama ambalo ni jambo nzuri,” afunguka.

Omar Zack, mmoja wa wateja wake anasema kuwa matibabu ya hijama yameimarisha afya yake pakubwa.

“Nilikuwa na maumivu katika sehemu za mwili wangu hasa kwenye viungo, maumivu ya kichwa, kizunguzungu, misuli kukosa nguvu na nilipotembelea kituo hiki, daktari akanieleza nasumbuliwa na uchovu (fatigue). Na tangu wakati huo hali yangu imeimarika na mimi huja kituoni kila mwezi kwa matibabu,” anasema.

Dkt Mohammed anasema kuwa kwa sasa anashughulikia mipango ya jinsi kutoa mafunzo ya matibabu haya ili kuweza kupanua biashara hiyo.

“Kwa sasa nimemfundisha binti yangu ambaye ana umri wa miaka 22. Hii ni kwa sababu wanawake wengi walikuwa wakiona ugumu kupokea matibabu kutoka kwangu,” anasema.

You can share this post!

Uhaba wa maji watatiza matibabu ya figo Lamu

Wanawake Pwani wahimizwa kugombea nyadhifa za kisiasa, wawe...

T L