• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
SHINA LA UHAI: Hofu magonjwa ya mdomo yakiongezeka nchini

SHINA LA UHAI: Hofu magonjwa ya mdomo yakiongezeka nchini

NA WANGU KANURI

JE, unapiga mswaki mara ngapi kwa siku?

Ikiwa wewe ni miongoni mwa maelfu ya Wakenya wanaosafisha mdomo mara moja kwa siku au baada ya siku kadhaa, unajiweka katika hatari ya kuandamwa na maradhi tele yanayoathiri mdomo.

Wataalamu wamependekeza watu kupiga mswaki mara mbili kwa siku.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza watu kutumia dawa ya meno yenye floridi, kusafisha meno kutumia uzi ili kuondoa uchafu katikati ya meno, kumtembelea daktari wa meno mara mbili kwa mwaka na kutotumia bidhaa zilizo na tumbaku kama njia ya kuhakikisha kuwa afya ya meno imeboreshwa.

Hali kadhalika, wazazi wanashauriwa kuhakikisha kuweka tu viwango vidogo vya dawa ya meno watoto wanatumia wanapopiga mswaki ili kuzuia kumeza dawa ile na kutema baada ya kusugua meno.

Afya ya mdomo ingali changamoto kwa mamilioni ya watu nchini licha ya maradhi yanayoathiri mdomo kuwa na tiba.

Ukosefu wa maarifa kuhusu afya ya mdomo pamoja na gharama ya juu ya matibabu ni mojawapo ya changamoto za utoaji wa huduma za afya ya mdomo. Afya hii hujumuisha meno, ufizi, ulimi viungo ambavyo humwezesha mtu kuzungumza, kutafuna na hata kutabasamu. Kula au kutumia vinywaji vilivyo na sukari nyingi, kutopiga mswaki na kuvuta au kutafuna tumbaku ni hatari kwa afya ya mdomo.

Ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa 194 duniani yaliyo na visa vingi vya ugonjwa wa fizi ambao huathiri tishu zinazozingira na kushikilia jino (periodontal gum disease), kuoza na kung’oka kwa meno na kansa ya mdomo.

Kulingana na Daktari Steven Mbeva, afisa wa afya ya mdomo katika hospitali ya Komarock Modern, Wakenya wengi huugua ugonjwa wa ufizi na kuoza meno.

Kutoboka meno (dental caries) husababishwa sio tu na ulaji wa vyakula au kutumia vinywaji vyenye sukari nyingi bali pia uwepo wa bakteria kwenye mdomo na kutosugua meno vizuri mtu anapopiga mswaki.

Mgonjwa wa kuoza kwa meno hulalamikia kuumwa na jino kila mara, maumivu mtu anapokunywa au kula chakula chenye sukari au kikiwa moto au baridi, shimo kwenye jino, madoadoa meupe, yenye rangi ya nyeusi au hudhurungi kwenye jino na uchungu unapotafuna.

“Hata hivyo, magonjwa ya ufizi huwaathiri Wakenya wengi bila kubagua umri,” anaeleza.

Watu kutoka familia ambazo hupata mapato ya chini, walemavu, wazee na wale wanaoishi vijijini hurekodi idadi kubwa ya wagonjwa wa aina tofauti za mdomo.

Duniani, watu asilimia 45 huugua magonjwa ya mdomo huku watatu kwa wanne wakitoka kwenye familia zenye mapato ya chini na wastani.

Dkt Mbeva anaeleza kuwa watu kutoka familia za mapato ya chini huzuru hospitalini tu wanaposhindwa kufanya kazi zao za kila siku kutokana na maumivu ya jino.

“Vituo vingi vinavyoshughulikia afya ya mdomo huwa jijini huku wanaoishi vijijini wakizuru hospitalini tu wanapopata maumivu ikilinganishwa na kila mara kama inavyoshauriwa,” anasema Dkt Mbeva.

Gharama ya juu ya dawa ya meno iliyo na madini ya floridi huchangia katika kutozingatia afya ya mdomo haswa ugonjwa wa kuoza meno.

Ripoti ya WHO, Global Oral Health Status, inaonyesha kuwa magonjwa ya mdomo yameongezeka kwa bilioni 1 kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, ishara kuwa watu wengi hawazingatii afya yao ya meno.

Duniani, wagonjwa wa kuoza meno ambao hawapati matibabu ni bilioni 2.5. Robo yao huwa na umri wa kati ya miaka 20 na 64. Bilioni 1 huugua kutokana na magonjwa ya ufizi mojawapo ya sababu kuu za kung’oka kwa jino.

Vile vile, kila mwaka visa 380,000 vya kansa ya mdomo hurekodiwa.Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kilieleza kuwa zaidi ya asilimia 40 ya watu wazima waliripoti maumivu mdomoni mwaka jana huku zaidi ya asilimia 80 wakilalamikia kupata mojawapo ya ugonjwa wa mdomo kabla kufika miaka 34.

“Zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa miaka 6 na 8 hulalamikia kuoza kwa jino angalau moja ya meno yanayochipuka baada ya kung’olewa.”Licha ya zaidi ya asilimia 90 ya watu duniani wakiugua magonjwa tofauti ya mdomo, gharama ya juu ya matibabu ni kizingiti cha kuendeleza afya.“Afya ya mdomo imepuuzwa kwa muda mrefu licha ya magonjwa mengi kuweza kudhibitiwa,” anasema Tedros Ghebreyesus, Mkurugenzi wa WHO.

You can share this post!

Hofu wasichana wateswa chuoni na ‘masponsa’

Aliyehukumiwa kifungo cha miaka 28 kwa mauaji awa huru

T L