• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 11:36 AM
TAHARIRI: Wachochezi wote wa ghasia wakabiliwe

TAHARIRI: Wachochezi wote wa ghasia wakabiliwe

KITENGO CHA UHARIRI

KISA AMBAPO msafara wa Naibu Rais William Ruto ulishambuliwa kwa kupigwa mawe katika eneo la Kondele, Kaunti ya Kisumu, Jumatano, kinapaswa kutuzindua kuhusu athari za ghasia za kisiasa.

Kwa muda mrefu, taswira ya siasa nchini imekuwa ikiandamwa na chuki za kikabila, mivutano baina ya wanasiasa na ghasia baina ya makundi ya kisiasa. Athari za vitendo hivyo imekuwa ni majeraha, watu kufurushwa makwao na hata maafa.

Upeo wa athari za chuki za kikabila ulishuhudiwa wazi mnamo 2007/2008, baada ya Wakenya zaidi ya 1,300 kuuawa huku wengine karibu 600,000 wakiachwa bila makao. Cha kushangaza ni kwamba, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa ghasia za kisiasa kufanyika nchini.Ghasia kama hizo ziliripotiwa baada ya chaguzi za 1992, 1997 na 2002.

Katika wakati ghasia hizo zote zilitokea, Wakenya wa kiwango cha chini ndio walikuwa waathiriwa wakuu. Hadi sasa, wengi wao bado ni wakimbizi wa ndani, baada ya tawala za awali kukosa kutimiza ahadi za kuwapa makao mbadala.

Chini ya kumbukumbu chungu kama hizo, imefikia wakati Wakenya waanze kutathmini mustakabali wao wa kisiasa kila wakati mwanasiasa anajitokeza kuwachochea kwa namna yoyote ile.Katika tukio la Kondele, wale waliohusika ni Wakenya wa kawaida, wala si watoto ama jamaa za wanasiasa wanaochochea wananchi kushiriki katika ghasia kama hizo.

Kinaya ni kuwa, wanasiasa hao huwa wanalindwa vikali na walinzi wao. Magari yao huwa ya kisasa, huku baadhi yao yakiwa hata na uwezo wa kuhimili makali ya risasi.Mavazi wanayovaa huwa si ya kawaida.

Kama magari yao, huwa yanahimili mashambulio ya aina yoyote ile. Uchaguzi Mkuu wa 2022 unapokaribia, ni lazima wananchi wafahamu wanasiasa watafanya kila wawezalo kujizolea umaarufu. Si mara moja wanasiasa wamesikika wakidai walipanga baadhi ya matukio ya ghasia kimakusudi ili kujizolea umaarufu wa kisiasa.

Hivyo, ni wazi kuwa tutashuhudia sarakasi nyingi kabla uchaguzi huo kuwadia. Cha muhimu kwa wananchi ni kufahamu kuwa ikiwa patazuka hali ambapo ghasia zozote zitatokea, wanasiasa hawatajitokeza hata kidogo kuwasaidia.

Kama awali, wao ndio watakuwa waathiriwa huku wanasiasa na washirika wao wakiendelea na maisha yao kama kawaida.Licha ya wito huu kwa wananchi, taasisi husika pia lazima ziwajibike kwa kuwachukulia hatua wanasiasa wanaoonekana wakiwachochea wafuasi wao kushiriki katika ghasia au kuwashambulia washindani wao.

Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) inapaswa kusimama kidete, kwa kuwashtaki wanasiasa hao badala ya kuwakashifu pekee.

You can share this post!

Raila ataka Chebukati kuomba Kenya radhi

Ruto amtupia Raila onyo kali kuhusu Nyanza

T L