• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Raila ataka Chebukati kuomba Kenya radhi

Raila ataka Chebukati kuomba Kenya radhi

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI WA ODM Raila Odinga sasa anamtaka mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, kuhakikishia Wakenya kuwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 utakuwa huru na wa haki.

Bw Odinga jana alisema pia anatarajia Bw Chebukati kuomba msamaha Wakenya kwa ‘kusimamia vibaya’ uchaguzi wa Agosti 8, 2017 ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu.Waziri Mkuu wa zamani ambaye anatarajiwa kutangaza rasmi azma yake ya kugombea urais Desemba 9, mwaka huu, alisema atakubali kushindwa katika Uchaguzi Mkuu ujao ikiwa utakuwa huru na haki.

“Kama uchaguzi utafanyika vyema – bila visa vya udanganyifu – na nishindwe, nitakubali matokeo. Asiyekubali kushindwa si mshindani.“Mimi nimewahi kuwa mchezaji wa mpira na ninajua vyema kwamba, ushindani ni mambo mawili:

kushinda au kushindwa,” Bw Odinga akasema katika mahojiano na vituo vya redio vinavyotumia lugha ya Kikamba.Bw Odinga alitoa wito huo kwa Bw Chebukati huku baadhi ya viongozi wa Jubilee wakimtaka mwenyekiti huyo wa IEBC kuondoka kutokana na madai kwamba, anaegemea mrengo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu wa Rais William Ruto.

“Bw Chebukati hana budi kuwahakikishia Wakenya kuwa Uchaguzi Mkuu ujao utakuwa huru na haki. Vilevile, namtarajia kuomba msamaha kwa kusimamia visivyo uchaguzi wa 2017,” akasema.Viongozi hao wa Jubilee, wakiongozwa na mbunge wa Nyeri Mjini Wambugu Ngunjiri, wanashuku kwamba Uchaguzi Mkuu huenda usiwe huru na haki.

Viongozi hao wa Jubilee walianza kutoa shinikizo za kutaka kumng’oa Bw Chebukati baada ya mwenyekiti huyo wa IEBC kuwashauri watumishi wa umma, wakiwemo mawaziri, kukoma kujihusisha na siasa za mirengo.

Bw Chebukati alitoa ushauri huo baada ya Dkt Ruto kumtaka kuwachukulia hatua mawaziri; Dkt Fred Matiang’i (Usalama) na Bw Joe Mucheru (Mawasiliano ya Teknolojia –ICT) kwa kutangaza wazi kuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais mwaka ujao.“Katika uchaguzi wa 2017, Bw Chebukati alisema hakuna makosa kwa mawaziri kujihusisha na kampeni za kisiasa.

Lakini mwaka huu amebadilika na anawataka wasijihusishe na siasa.“Inaonekana Bw Chebukati anazungumza lugha ya UDA. Ajiuzulu aende ajiunge na UDA kwani hatuamini kwamba ataendesha uchaguzi huru na haki,” akasema Bw Wambugu.Shinikizo hizo za viongozi wa Jubilee kutaka kumng’oa Bw Chebukati zimezua hofu katika kambi ya Naibu wa Rais kwamb,a huenda ni njama ya kutaka kuiba kura mwaka ujao.

“Mbona Jubilee wanashinikiza mwenyekiti wa IEBC kuondoka sasa? Tunawashuku sana,” akasema Bi Millicent Omanga, Seneta Maalum, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.Septemba, mwaka huu, viongozi wa ODM walisitisha juhudi zao za kutaka kumng’oa Bw Chebukati.

Awali, mwenyekiti wa ODM John Mbadi na Mwakilishi wa Wanawake wa Homa Bay, Gladys Wanga walikuwa wamemtaka Bw Chebukati kujiuzulu huku wakidai hawana imani naye.Lakini baadaye, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema shinikizo za viongozi hao wawili kutaka kumng’oa Bw Chebukati hazikuwa msimamo wa chama hicho

You can share this post!

Wanjigi aelezea imani atambwaga Raila na kubeba bendera ODM

TAHARIRI: Wachochezi wote wa ghasia wakabiliwe

T L