• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Ruto amtupia Raila onyo kali kuhusu Nyanza

Ruto amtupia Raila onyo kali kuhusu Nyanza

GEORGE ODIWUOR na DANIEL OGETTA

NAIBU RAIS William Ruto amemwambia kinara wa ODM, Raila Odinga, na wawaniaji wengine wa urais kujitayarisha kwa kivumbi kikali katika eneo la Luo Nyanza.

Katika juhudi za kuwarai wenyeji kumuunga mkono 2022, Dkt Ruto alisema atakuwa akifanya ziara za mara kwa katika eneo hilo, linalochukuliwa kuwa ngome ya kisiasa ya Bw Odinga.Alisema atafanya ziara nyingine kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mikakati hiyo inalenga kuimarisha uhusiano wake na wenyeji, ambapo idadi kubwa haijakuwa ikimuunga mkono.Alisema atakuwa akizuru katika kaunti za Kisumu, Homa Bay na Migori ili kupata uungwaji mkono kutoka kwa wenyeji, ambao wamekuwa wakimpigia kura Bw Odinga kwa muda mrefu.

“Hii si ziara ya wakati huu pekee. Ninalenga kujenga urafiki baina ya eneo la Nyanza na maeneo mengine nchini,” akasema.Dkt Ruto hajakuwa akifanya ziara katika eneo hilo, licha ya kuonekana kuvumisha azma yake ya urais katika sehemu nyingine nchini.

Kwa mfano, alifanya ziara ya mwisho katika Kaunti ya Homa Bay mnamo 2017, alipoandamana na Rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Mbita. Wakati huo, walikuwa wakifanya kampeni za Chama cha Jubilee (JP) kuwarai wenyeji kumpigia kura Rais kwenye uchaguzi wa 2017.

Jana, Dkt Ruto alipokelewa vizuri katika vituo vya kibiashara vya Kendu Bay, Adiedo Kadel na Olare. Mapokezi hayo yalionekana kumshawishi Dkt Ruto kubuni mipango ya kufanya ziara zaidi katika eneo hilo.

Dkt Ruto alisema atazuru maeneo mengine katika kaunti hiyo, akiongeza kuwa kila mtu yuko huru kuzuru mahali popote nchini.Akizungumza baada ya kukutana na viongozi wa chama cha UDA mjini Homa Bay Jumatano usiku, Dkt Ruto alisema analenga kuboresha uhusiano wake na wenyeji anapojitayarisha kuwania urais 2022.

“Kuna dhana kwamba eneo la Luo Nyanza haliwezi kunipigia kura. Binafsi, siwezi kukubali dhana kama hizo. Ni sababu hiyo ambapo nipo huku,” akasema.Vile vile, alisema kuwa kando na kuwarai wenyeji kumuunga mkono, hilo pia linalenga kuondoa dhana kuwa wenyeji huwa hawawakumbatii na kuwakaribisha viongozi kutoka maeneo mengine nchini.

Dkt Ruto na wanasiasa wengine wanaoonekana kuwa wapinzani wa Bw Odinga hukabiliwa na wakati mgumu wanapowahutububia wenyeji.Tukio la juzi zaidi lilishuhudiwa Jumatano, wakati Dkt Ruto alilazimika kukatiza hotuba yake katika eneo la Kondele, baada ya umati aliokuwa akiuhutubia kumgeukia.

Baadhi ya watu hata walirushia mawe msafara wake wa magari.Mwaniaji urais Jimmy Wanjigi pia alijikuta katika hali kama hiyo.Dkt Ruto alisema anaamini ziara zake zitaondoa siasa za ghasia na ukabila.

Aliwalaumu washindani wake kwa kutumia ghasia.“Hawana ajenda za kuwaeleza washindani wao. Kutokana na hilo, huwa wanatumia ghasia ili kuwatia hifu washindani wao,” akasema.“Kama wanasiasa, sisi ndio tumebuni dhana kwamba watu wengine wenye miegemeo tofauti ya kisiasa hawawezi kuruhusiwa kuhutubu eneo la Nyanza.

Nitahakikisha dhana hiyo imeisha,” akaongeza.

You can share this post!

TAHARIRI: Wachochezi wote wa ghasia wakabiliwe

Bidhaa: Maafisa walaumiwa kwa kuzembea

T L