• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
TALANTA: Dogo anayetamba katika muziki wa ala na sarakasi

TALANTA: Dogo anayetamba katika muziki wa ala na sarakasi

NA PATRICK KILAVUKA

ANASEMA kusoma na kuelewa arudhi na tamrini za usanii wa muziki na uanasarakasi kunahitaji uelewa wa lugha.

Yeye hupenda kucheza muziki wa ala ambao unaimbwa haswa kwa lugha Kiswahili mbali na Kiingereza.

Anakariri kwamba msanii anafaa kuwianisha fani anazopenda kwa kuelewa upesi njia ya kuafikia malengo yake katika usanii uwe wa muziki au sarakasi. ?Aidha, anazamia kuwa mwanamuziki siku za majaliwa.

Joseph Mwangi,13, mwanafunzi wa Darasa la Saba shule ya msingi ya Tumshangilieni Mtoto Education Centre, Kibagare, Kaunti ya Nairobi, ana weledi wa kucheza ala ya koneti na hushiriki pia michezo ya kubofyabofya viungo haswa akiendesha baiskeli na kuunda minara kuenda juu.

Mwanasarakasi Joseph Mwangi akionyesha jinsi ya kuendesha baiskeli huku akisawazisha mizani kwa kubeba mwenzake wa kikundi cha sarakasi shuleni wakati wa mazoezi. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Mbali na kutoka kambini akitumia baiskeli, anasema uelewa wa lugha ya mkufunzi na kufuata maagizo ndicho kimekuwa kigezo cha kufaulu kwake katika fani ya sarakasi na kucheza ala.

“Pasi na kujua lugha, huwa vigumu kusoma muziki ukicheza,” asema msanii huyo ambaye muziki huwa njia ya kuwasiliana, kufunzana, kuelimisha na kutumbuiza.

Aidha, sarakasi huwa pia mwanya wa kujisawazisha kimawazo na kutumbukia.

Alianza pilkapilka za usanii wa muziki ala na sarakasi mwaka 2019 akiwa darasa la nne akiwa chini ya wakufunzi Kennedy Kirvwa (muziki) na Peter Wainaina (sarakasi).

Anadokeza mazoezi ya Jumatatu, Jumatano na Ijumaa yamekuwa nguzo yake ya kuinuia vipaji hivi na sasa anaona matunda ya kuvitilia maanani.Amejua mbinu mbambali ya sarakasi, hususa kuendesha baiskeli akijibofyabofya pamoja na kusawazisha mizani. Isitoshe, anaweza kuimba muziki ala.

Hutumia maarifa ya muziki wa ala kuimba wimbo wa kitaifa, Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata za mataifa mengine kwani amekuwa katika bendi ya shule hiyo ambayo imewahi kushiriki katika hafla mbalimbali.Akiwa na kikundi cha wanasarakasi hualikwa kwenye hafla za kutumbuiza pamoja na za shuleni.

Joseph anasema vipawa vyake vimemfungua kimawazo, kuimarisha ujasiri na kuwa mbunifu katika kubuni maarifa ya kucheza muziki wa ala na kuibua msisimuko wa uanasarakasi.?Walimu wake walikiri kwamba, amekuwa mwepesi sana kuelewa kufanya sarakasi na kucheza muziki wa ala.

“Ilimchukua karibu mwezi mmoja kushika laini,” akiri mmoja wa wakufunzi wa talanta.

Wakufunzi wake wanamuaminia katika kutelekeza wajibu.

Pia, walimdokeza kuwa mraibu mkuu wa fani zake kwani anapenda kujinoa bila kusukuma hali ambayo imekuza ari na kumakinika kwake.

Joseph anasema changamoto ambayo alikuwa nayo katika kucheza ala ni kuhimili uchezaji kwa muda mrefu kwani, chombo hiki ni kile inahitaji hewa na nguvu nyingi ndiposa ufanikiwe kukicheza.

Aidha sarakasi huhitaji usawizishaji wa mizani ndiposa uepuke kujeruhiwa.

Anasema angependa kutumia vipaji hivyo kumfungulia milango ya heri siku za majaliwa na amekuja kutambua usije ukaudharau mwanzo wako mdogo kwa sababu huo ndio unakuundia barabara ya taaluma au ajira.

Isitoshe, anaarifu kwamba kuelewa usanii kwahitaji uelewe lugha inayotumiwa,kuwa na nidhamu, bidii ya mchwa katika kujitolea na ushirikiano sako kwa bako wadau husika.

Hatimaye anatoa mkono wa tahania kwa mkurugenzi wa shule Japheth Njenga kwa vifaa wanavyotumia kukuza talanta zake na walimu wake kwa kulea vipaji vyake.

You can share this post!

Kasikasi FC, Kisa FC na Melta Kabiriah Youth ndio mabingwa...

Wafanyabiashara washiriki kongamano la maonyesho ya bidhaa...

T L