• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
TALANTA: Wembe katika sataranji

TALANTA: Wembe katika sataranji

NA CHRIS ADUNGO

KUBWA zaidi katika matamanio ya Jimnah Ngugi ni kuwa mchezaji maarufu wa sataranji (chess) kiasi cha kumfikia bingwa mara tano wa dunia katika mchezo huo, Magnus Carlsen kutoka Norway.

Wanaozidi kuweka hai ndoto ya mwanafunzi huyu mwenye umri wa miaka minane ni mamake mzazi, Bi Magdalene Wanjiru, na kocha wake wa sataranji, Bw Theuri Boniface Njogo.

Mbali na nduguze – Purity na Gibrath Gitau; mwingine anayemhimiza Jimnah katika mchezo huu wa kufikirisha ubongo ni mjomba wake, Bw Zachary.

“Kipaji cha kucheza sataranji kilianza kujikuza ndani ya Jimnah akiwa na umri mdogo sana. Alipenda sana kuchora. Vyombo vya kidijitali vilimsisimua mno na alivutiwa zaidi na vibonzo na michezo iliyoshirikisha viwango vya juu vya ubunifu wa kiteknolojia,” anasema Bi Wanjiru.

“Zaidi ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi, anapenda pia masomo yanayoegemea sanaa na mawasiliano. Ni mwanafunzi wembe ambaye huongoza darasa lake katika kila mtihani,” anasema Bw Njogo – Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ya NJ’s Christian (Njiraini’s), Kahawa West, Nairobi.

Weledi wa Jimnah katika sataranji uliwahi kumpa fursa ya kuwakilisha Kenya katika michezo ya African Youth Chess Championships nchini Zambia mwanzoni mwa Julai 2022.

Hiyo ilikuwa baada ya kubwaga zaidi ya wavulana 200 na kutinga orodha ya 10-bora kitaifa katika kategoria ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka minane.

Mwanafunzi huyu wa gredi ya tatu alizoa pointi tano kati ya saba katika mashindano hayo ya Kenya National Youth & Cadets Chess Championships jijini Mombasa mnamo Aprili 2022.

Awali, alikuwa ametamalaki makala ya kwanza ya kipute cha Visa Oshwal Chess Championships jijini Nairobi kwa kuzoa pointi tano kati ya sita.

Alijishindia nishani ya dhahabu katika mapambano hayo yaliyojumuisha wavulana 82.

Jimnah alitia fora zaidi katika kipute cha Nairobi Open Youth Chess kilichofanyika katika shule ya msingi ya Riara Springs wikendi iliyopita.

Alikuwa miongoni mwa wavulana 100 kutoka shule 10 mbalimbali za Kaunti ya Nairobi walionogesha kategoria ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 10.

“Mashindano ya sampuli hii na mengine ya ndani kwa ndani ambayo huandaliwa shuleni yamekuwa majukwaa mwafaka kwa Jimnah kutononoa kipaji chake. Sasa analenga kushiriki mapambano ya World Youth Chess Championships na kutamba katika kipute cha kila mwaka cha African Schools Individual Chess Championships,” anaeleza Bw Njogo.

Ingawa kwa kawaida ni mpole na mnyamavu, Jimnah ana ukakamavu wa kuajabiwa katika mchezo huu unaohitaji akili pevu ili kumpiku mpinzani. Kinachoridhisha zaidi mkufunzi wake ni ujasiri wa Jimnah wa kukabiliana na kubwaga wachezaji wazoefu wanaomzidi umri.

“Ana ujuzi wa kuwasoma wapinzani wake na amepata umaarufu miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzake. Ana ari ya kuwaelekeza watoto wengine katika sataranji na inatia moyo kwamba anazidi kutambulika kimataifa,” anasema Bi Wanjiru.

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Mishahara ya walimu wa daraja la chini...

Matumaini idadi ya watalii watakaozuru Maasai Mara...

T L