• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tumuige Mtume kutimiza ahadi zetu kikamilifu

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tumuige Mtume kutimiza ahadi zetu kikamilifu

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Subuhaanahu Wataala, Mola wa viumbe wote duniani na akhera.

Swala na salamu zimwendee Mtukufu wa daraja, Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam.

Mtume huyu alikuwa kielelezo bora katika utekelezaji wa ahadi na kila muumin hana budi ila kujitahidi kutimiza ahadi anazotoa.

Hii ni miongoni mwa sifa tukufu na maadili mazuri.

Jambo hilo lilikuwa moja katika ada za Mjumbe wa Allah-Mtukufu-Swalla Llaahu alayhi wasallama, ambaye alikuwa akirejesha jambo jema kwa tukufu zaidi.

Wakati Hercules, mfalme mkristo aliwauliza waasi wa Kikuraishi kuhusu sifa za aliye Mtukufu wa daraja – Swalla Llaahu alayhi wasallama: “Je, yeye huvunja ahadi?” Wao walijibu: “Hapana!” Yeye akawaambia: “Vivyo hivyo Mitume hawavunji ahadi.”

Mtume huyu mtukufu alijali sana utekelezaji wa ahadi kwa Makureshi kiasi cha wao Makureshi kuvunja ahadi naye; lakini yeye alitekeleza ahadi hata baada ya watu wale aliowekeana nao ahadi kufariki.

Katika ubora huo, yeye alionyesha kiwango cha juu cha utekelezaji wa ahadi kwa mke wake wa kwanza mama Khadija-Radhiya Llaahu anha – alihifadhi nafasi na hadhi yake.

Alikiri nafasi yake kwake na kuendelea kuwakirimu rafiki na jamaa wa karibu.Mama Aisha-Radhiyallaahu anha, aliyekuwa mke wa Mtume-Swalla Llaahu alayhi wasallama, anasimulia kuhusu utimizaji wa ahadi za Mtume kwa mkewe wa kwanza, mama Khadija-Radhiyallaahu anha, aliyefariki muda mfupi baada ya kupewa Utume.

Mama Aisha-Radhiyallaahu anha hakupata kumfahamu na anasema: “Mtume alikuwa akimtaja sana Khadija na wakati mwingine alikuwa akichinja mbuzi na kukata nyama yake na kisha kuwagawia marafiki wa Khadija.

“Wakati mwingine nilikuwa namwambia, ‘Unafanya kana kwamba hakuna mwanamke mwingine duniani isipokuwa Khadija?’ “Na hapo yeye alisema: ‘Kwa hakika Khadija alikuwa hivi na hivi…na kuanza kutaja mazuri yake’.”

Wakati fulani Mtume-Swalla Llaahu alayhi wasallam alipokea ujumbe kutoka kwa An-Najashi; mfalme wa Ethiopia aliyewapokea na kuwalinda waislamu walipohamia huko katika ile Hijra ya kwanza.

Mtume alisimama na kuwahudumia mwenyewe, maswahaba zake wakasema: “Sisi tutafanya hayo!” Yeye akasema: “Hawa waliwakirimu maswahaba zangu nami ninapenda kuwalipa.”

Pamoja na hayo, Mtume wetu alikuwa mkweli kwa watu wake wa karibu pamoja na maswahaba zake.

Hakupata kusahau namna Abu Twalib alivyomlea kutoka umri wa miaka minane na kumlinda dhidi ya maadui wake.

Alitamani sana kuongoka kwake hadi mwisho wa maisha yake. Aliendelea kumuombea msamaha kwa Allah – Mtukufu hadi pale alipokatazwa.

Mfano wa jinsi Mtume alivyotekeleza ahadi kwa maswahaba zake ni lile tukio la Hatwib bin Abi Baltaa, pale alipotoa siri ya Mtume-Swalla Llaahu alayhi wasallam.

Lilikuwa kubwa na la hatari lakini Mtume alimsamehe kwa kukumbuka mema ya awali na hasa vita vya Badr.

Kwa hakika Mtume alionyesha mifano mingi katika nyanja zote za maisha yake, akitekeleza amri ya Allah-Mtukufu na kufuata tabia za manabii waliomtangulia.

Akawaambia maswahaba zake waliotaka kutekelezwa kwa adhabu dhidi ya Baltaa.

“Hakika yeye alishiriki vita vya Badr na unajuaje kama Allah-Mtukufu Hakuwaangalia watu wa Badr, Akasema fanyeni mtakavyo kwani mmesamehewa.”

Kwa hakika Mtume Muhamad – Swalla Llaahu alayhi wasallama alionyesha mifano mikubwa ya kimaadili katika nyanja zote za maisha yake akitekeleza amri ya Allah-Mtukufu na kufuata tabia za manabii waliomtangulia.

You can share this post!

DOMO KAYA: Ukimya ni dhahabu…!

TAHARIRI: Magavana walipe madeni ya kaunti

T L