• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 2:33 PM
DOMO KAYA: Ukimya ni dhahabu…!

DOMO KAYA: Ukimya ni dhahabu…!

Na MWANAMIPASHO

DUH! Wajua bwana kuna mambo mengine kama mwanaume unatakiwa kukaa kimya.

Imefikia hatua sasa tunashindana na wenzetu wa kike kwa sifa ambazo hatukujaliwa nazo.

Kwa kawaida watu wenye sifa ya kuzungumza na kutupia maneno ni wanawake.

Ndio hulka yao. Ila sasa tunao wanaume wanaoiga tabia hizi.

Mfano mzuri huyo mchekeshaji wenu kipenzi Eric Omondi.

Sikutegemea kabisa kuyasoma yale aliyoyaibua.

Jomba kadri anavyokaribia kutimiza umri wa miaka 40, ndivyo mawazo yanazidi kumtoka au kumwishia sijui.

Ungetegemea kumwona zaidi mtu mkomavu ila unayemwona ni zumbukuku.

Mawazo yake hayaeleweki.

Mwanzo kabisa nashindwa kuelewa ni kwa nini aliamua kumdhalilisha Jacque Maribe kivile.

Na hata nikiamua kutomkingia Maribe, bila shaka nitamkingia yule mtoto.

Mtakuwa mnafahamu kinachoendelea baina yao. Aliyeanza yote ni Eric, kumbe ulikuwa ni mtego wa kwake kufungua uwanja wa kurushiana cheche.

Imenisikitisha kwa kweli. Yule mtoto hakustahili kabisa haya atakayokuja kuyaona mitandaoni atakapokuwa mtu mzima. Ameishi kujua Eric ndio babake ila baada ya miaka saba jamaa akaruka.

Ikiwa Maribe aligoma mtoto afanyiwe DNA, hivi basi ni kwa nini alikubali awali kujihusisha na maisha ya mtoto huyo hadi akawa anawapeleka kula bata kwenye maeneo ya kifahari?

Leo aamke na kudai Maribe amekuwa akimzungusha kwa miaka saba kila alipoomba wafanye DNA.

Khu! Sitaki kuendelea sana sababu hii ni moja ya zile mada ambazo zinasinya sana hasa pale mtoto anapohusishwa. Ila nimehakiki Eric huenda akawa ana tatizo la kiakili kwa namna anavyofanya drama zake hizi.

Lakini leo sipo kwa Eric, mawazo yangu yote yapo kwa Pasta James Ng’ang’a.

Ng’ang’a au ukipenda jinsi anavyopenda kujichocha mwenyewe, mwite Chief General Commander. Juzi nimesikia kajiongezea lakabu nyingine, Kenya Air One. Ng’ang’a sio mgeni kwa wengi. Drama na vituko vyake vinatosha kuandika vitabu 12.

Sasa juzi Baraza la Vyombo vya Habari Nchini-MCK, limempa onyo la kuchukulia hatua kali kituo chake cha televisheni, Sasa TV kwa kauli chafu alizotoa hewani.

Kwenye mojawapo ya mahubiri yake yaliyopeperushwa runingani, jamaa alionya siku akifa, manesi wasijaribu kuugusa mtarimbo wake.

Kauli hiyo ndio imepelekea MCK kumtumia onyo. Sasa jamaa kwa ile hulka yake ya ujeuri na kiburi kawajibu. Anachotaka wafahamu ni kwamba, wao sio mabosi wake.

Mabosi wake pekee ni Halmashauri ya Mawasiliano Nchini (CAK) ambao tayari anasema wameshamwona.

Kwa MCK, amewataka wafahamu kuwa yeye ni muhubiri na wala hana muda nao na hawapaswi kumwambia chochote kuhusu TV yake.

Na ikiwawasha sana, amewaambiwa wanaweza kuuza kondomu wakitaka ila yeye wamwache kama alivyo sababu kama CAK hawajamkanya, basi wao ndio nani.

Sitataka kuingilia vita vya Ng’ang’a sababu ni jamaa mmoja fulani wa kiajabu.

Ila ninachoweza kusema ni hiki, wengi wetu tunamfuata kwa sababu hana tofauti na wachekeshaji. Kauli zake hizo wakati mwingine hutulegezea siku mambo yanapokuwa magumu.

Ndio sababu tunamfuatilia.

Mtakubaliana nami kwamba, asilimia kubwa ya mafunzo yake Ng’ang’a, hakuna ambaye huyafuatilia ila ni zile dondoo ambazo jamaa huangusha.

Binafsi nampendea hilo. Huwa ananichangamisha sana.

Kwa sasa acha nimsubiri Chief General Commander arejee kutoka Marekani aje kupambana na MCK.

You can share this post!

WASONGA: Likizo si suluhu, ni sawa na kutibu malaria na...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tumuige Mtume kutimiza ahadi zetu...

T L