• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
UFUGAJI: Wachina huwania nyama ya sungura wao kila wakati

UFUGAJI: Wachina huwania nyama ya sungura wao kila wakati

NA PETER CHANGTOEK

UFUGAJI wa sungura ni shughuli ambayo inaweza kumfaidi mfugaji, hasa iwapo ataiendeleza kwa njia ifaayo.

Sungura wana manufaa; mbali na kuuzwa wakiwa hai na kutia kibindoni hela, mfugaji hupata nyama, ngozi na mbolea.

Aidha, shughuli hiyo haihitaji nafasi kubwa au shamba kubwa ili kuiendeleza. David Kinyanjui na mkewe Rose walijitosa katika shughuli hiyo 2021. Wamekuwa wakiuza sungura, nyama, mbolea – mkojo na kutumia ngozi kutengeneza bidhaa aina ainati.

Wanamiliki shamba linalojulikana kama Daroclael Rabbit Farm katika eneo la Dagoretti, Nairobi. Waliliunda jina Daroclael kutoka kwa herufi za kwanza za majina yao.

“Da – David, husimamia mume wangu, Ro – Rose, Cla – Clare – kifunguamimba wetu na El – kitindamimba wetu ambaye ni Elsie,” aeleza Rose.

Anadokeza kwamba walitumia mtaji wa Sh600,000 kuanzisha shughuli hiyo, hela zilizojumuisha gharama ya ujenzi wa vibanda na ununuaji wa sungura walioanza nao.

“Tulianza Januari 2021 kwa sungura 20 wa kike na 10 wa kiume. Tuliwanunua kutoka Ngong kwa Sh750 kila mmoja,” asema, akiongeza kuwa, waliwanunua wa kike waliokomaa kwa Sh2,500 kila mmoja.

Hata hivyo, baadhi yao walikufa kwa sababu ya kuwalisha lishe nyingi kupita kiasi.

Wao huwafuga sungura spishi nyingi, mathalani: New Zealand, California white, Dutch, Checkered, Chinchilla, Havana na Flemish Giant.

Anaongeza kuwa, mwaka uliopita kulikuwa na ukosefu wa lishe, na wakashauriwa wawalishe aina ya hay zilizotengenezwa kwa mabua ya mpunga na wimbi, jambo lililosababisha kufa kwa sungura takribani 100.

Huwauza sungura wenye umri kuanzia miezi mitatu hadi minne. Huuza kilo moja ya nyama ya sungura kwa Sh700.
Wengi wa sungura wao huwa na uzani wa kilo 1.2 na 1.5. Hata hivyo, wale waliokomaa sana wanaweza kuwa na uzani wa kilo 2.

Rose anadokeza kuwa, hawataki kuwafuga hadi wawe na uzani mwingi kwa sababu watalazimika kutumia fedha nyingi kwa lishe.

Kinyanjui na mkewe huuza nyama ya sungura kwa hoteli moja ya Wachina iliyoko katika eneo la Hurlingham, Nairobi, japo wanasema kwa bei ya chini mno.

Huuza kilo moja ya nyama kwa Sh450. Hata hivyo, wateja hao baadaye huuza kilo moja ya nyama hiyo kwa bei ya Sh900. Wao huwachinja na kupakia nyama na kuwapelekea wateja hao.

Rose anafichua kwamba, huuza sungura takribani 20 kwa muda wa majuma mawili. Mojawapo ya changamoto ambazo wamezipitia katika ufugaji wa sungura ni bei ghali za lishe.

Kuna wakati ambapo walikuwa wakinunua lishe aina ya hay kwa Sh500. Hata hivyo, anasema kuwa bei hiyo imepungua hadi Sh350.

Aidha, anasema kuwa hununua lishe za madukani aina ya pellets kwa Sh2,350, japo kuna wakati ambapo walikuwa wakinunua kwa Sh2,400 kwa gunia la kilo 50.

Wao hukusanya mbolea na mkojo wa sungura na kuuza.

“Hupata karibu lita 20 za mkojo kwa siku,” asema Kinyanjui, akiongeza kuwa, wana sungura takribani 350.

Kinyanjui anaongeza kuwa, kuna wakati ambapo walikuwa na sungura wengi na wakati huo, walikuwa wakipata lita 40 za mkojo wa sungura kila siku.

Anafichua kuwa, huuza lita moja kwa Sh100. Aidha, huuza mbolea kwa Sh3,000. Lita moja ya mkojo huo, Kinyanjui adokeza, huchanganywa na maji lita mbili.

Anasema kuwa, huku mashamba yanapoendelea kuwa madogo kwa sababu ya idadi ya watu inayoendelea kukua, ufugaji wa sungura waweza kuwa chaguo aula.

David Kinyanjui na mkewe Rose wakionyesha bidhaa wanazozitengeneza kwa ngozi ya sungura. PICHA | PETER CHANGTOEK

Pia, anapendekeza kuwa, ni muhimu iwapo bei za sungura zingesawazishwa kila mahali, ili kuboresha shughuli hiyo.

Anafichua kwamba, ana mipango ya kuwa na kituo cha kuuzia nyama ya sungura katika siku zijazo.

Rose hutumia ngozi za sungura kuzitengeneza bidhaa kama vile; mikeka midogo na kuiza kwa Sh300-Sh600 kwa marafiki na wateja wengineo.

Anawashauri wale wanaonuia kujitosa katika ufugaji wa sungura kuanza kwa idadi ndogo na kuongeza idadi kadiri muda unavyosonga.

“Wengi wa wafugaji wa sungura ni ‘mahasla’ na wanateseka. Ninaomba rais kuwasaidia wafugaji kupata mafunzo na kuwa na mahali pa kuchakata ngozi na mahali pa kuwachinjia,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Joto la kisiasa lapanda Tanzania Lissu akirejea

ZARAA: Aliachana na mahindi kahawa iliponyanyuka

T L