• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
VITUKO: Suala la chanjo kwa walimu lawa kiazi moto katika nchi ya Kavaluku

VITUKO: Suala la chanjo kwa walimu lawa kiazi moto katika nchi ya Kavaluku

Na SAMUEL SHIUNDU

ULIKUWA umetimu mwaka sasa tangu kisa cha kwanza cha mwathiriwa wa virusi vya Corona kiripotiwe nchini Kavaluku.

Ilisadifu kuwa wakati wa maadhimisho hayo nchini, ulimwengu wote ulikuwa umetikiswa na awamu ya tatu ya maambukizi. Mtikiso huu uliwatia watu wa Kavaluku katika hofu kuu. Kila kuchao, ripoti zilionesha kuwa idadi ya walioambukizwa na waliofariki iliendelea kuongezeka kama zebaki kwenye kipimajoto. Hofu iliutawala kila moyo wa mwanakavaluku.

Hofu hii iliwafanya baadhi yao waliokuwa wakiipinga chanzo kuanza kuilegeza misimamo yao. Hata hivyo, walichelea kuiendea chanjo hii ambayo ilikuwa imeachiwa hohehaje wa Mungu. “Mimi si masikini yakhe!” Sindwele alimwambia mlevi mmoja aliyejaribu kumuuliza Kama alikuwa kapokea chanjo.”Suala kuhusu chanjo kawaulize mburumatari wengine huko!” aliongezea.

“Kwani wewe si mwalimu?” Nafoyo alimuuliza kana kwamba maskini kilikuwa kisawe cha mwalimu. “Samahani mwalimu lakini nilisikia kuwa nyinyi mlipaswa kupokea chanjo kwenye awamu hizi za mwanzomwanzo.” Nafoyo alijibu baada ya kushuku kuwa alikuwa kamkuna mteja wake pabaya.

“Walisema hivyo lakini wenyewe hawajichanji.” Sindwele alilalamika.

“Lakini Mwalimu hebu kawazie. Nyinyi ni kioo chetu, sasa mkiikataa chanjo hii ni nani ataikubali? Wanasema kuwa mganga hajigangi. Lazima walimu mgangwe kwanza ndipo walalahoi kama sisi tufwate.” Nafoyo alimweleza mwalimu Sindwele.

“ Kweli mama.” Mmoja wa wateja alimuunga mkono jabla ya kumgeukia Sindwele na kumwonya, “Wajua siku hizi lazima tuchunge kazi tulizojaliwa zisije zikatuponyoka.”

“Kama chanjo hiyo ndiyo itafanya nipoteze kazi, nitastahabu kuipoteza kazi hiyo.” Sindwele alijitia kiburi.

“Na ukiipoteza kazi hiyo, utayalipaje madeni yangu?” Nafoyo alimchokoza mwalimu. Sindwele aliyaweka maneno ya mgema wake kwenye mizani. Japo yalimuuma, yalikuwa na ukweli fulani. Alizoea kupata vinywaji hapo kwa mkopo na kuvilipia mwishoni mwa mwezi. Kupoteza kazi kungemletea balaa. Akaufyata na kupiga kopo la kangara. Hakupenda mkondo ambso mazungumzo hayo yslikuwa yameanza kuchukua. Hakuna aliyemwelewa katika kundi lile, ‘wanajua nini mahambe Hawa zaidi ya kulewa?’ alijiwazia kuwahusu wenzake.

Aliacha kushiriki mjadala huo. Badala yake akaanza kuiwazia barua aliyokuwa kapokea Jana yake. Alikuwa kapata mwaliko wa kwenda kusahihisha mtihani wa kitaifa. Mwaliko huo ulimweka katika njia panda. Hakuwa na uhakika wa usalama wa afya yake katika vituo hivyo vya usahihishaji. Wakati huo huo, alihitaji vijihela hivyo vikamfae kulipia hayo madeni aliyokuwa kakumbushwa na Nafoyo.

You can share this post!

USWAHILINI: Mnara wa pembe jijini Mombasa ndio nembo kuu ya...

NDIVYO SIVYO: ‘Kuwa’ na ‘kua’ yana ukuruba tu wa...