• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
VYAMA: Chama cha Uanahabari katika shule ya upili ya Mbirikene, Meru

VYAMA: Chama cha Uanahabari katika shule ya upili ya Mbirikene, Meru

NA CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Uanahabari katika shule ya upili ya Mbirikene iliyoko Imenti Kaskazini, Kaunti ya Meru, kinashughulikia mahitaji ya wanafunzi wenye ari ya kujikuza katika taaluma za utangazaji wa habari, uhariri, tafsiri na ukalimani.

Wanachama huzamia utafiti kila kukusanya makala na habari za matukio mbalimbali ndani na nje ya shule, kuzihariri na kuziwasilisha gwarideni kila Jumatatu na Ijumaa.

Lengo jingine la chama ni kupiga jeki shughuli za Idara ya Lugha ili kuboresha matokeo ya mitihani ya KCSE na kuwapa wanafunzi majukwaa mwafaka ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vyao katika sanaa anuwai kama vile ulumbi, uimbaji na uandishi wa kazi bunilizi.

Chama kwa sasa kipo chini ya ulezi wa Bi Mediatrix Sakwa ambaye hushirikiana kwa karibu na Bw Bundi Marete (Mwalimu Mkuu), kuratibu shughuli muhimu za chama kila muhula.

Wanachama hukutana mara kwa mara baada ya vipindi vya masomo jioni ili kujadili maendeleo ya chama na kuzamia na masuala mengine ya kiakademia.

Ari ya kutaka kujikuza katika tasnia ya uanahabari, nidhamu ya kiwango cha juu na wepesi wa kujituma kwa kushiriki kikamilifu shughuli zinazochangia makuzi ya lugha; ni miongoni mwa vigezo muhimu vya kujiunga na chama hiki.

Chama kwa sasa kina mikakati ya kuchapisha jarida rasmi la shule na kushiriki shughuli za kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo kutembelea mayatima, kuhifadhi mazingira na kuwasaidia wasiojiweza.

“Chama kinalea vipaji vya wanafunzi katika sanaa na fani tofauti zinazofungamana na masomo ya lugha. Zaidi ya kuwakuza kimaadili, wanafunzi wengi wameamshiwa hamu ya kuwa wanahabari,” asisitiza Bi Sakwa.

  • Tags

You can share this post!

Muyoti aanza kupanga City Stars upya

Maseneta wa Azimio wamkosoa Ruto kuhusu GMO

T L