• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 3:36 PM
VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili chuoni Laikipia ni jukwaa la uhakika katika makuzi ya lugha na vipaji

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili chuoni Laikipia ni jukwaa la uhakika katika makuzi ya lugha na vipaji

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Laikipia (CHAKILA) kilianzishwa mnamo 2013 chini ya mwavuli wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA).

Lengo mahsusi la chama ni kuwapa wanafunzi jukwaa maridhawa la kukichapukia Kiswahili na kuboresha utangamano wa kitaifa na kimataifa kupitia tamaduni mbalimbali za Kiafrika.

Kufikia sasa, chama kinajivunia zaidi ya wanachama mia moja kutoka vitivo mbalimbali japo idadi kubwa ya wanachama ni wanafunzi wanaosomea kozi za ualimu na uanahabari.

Wapo viongozi walioteuliwa na kuchaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama ili kushikilia nyadhifa mbalimbali chini ya usimamizi wa Dkt Sheila Wandera-Simwa ambaye ni mlezi wa chama.

Chama pia kinapata malezi na ushauri wa mara kwa mara kutoka kwa Prof Onyango Ogola, Prof Aswani Buliba na Bw Henry Indindi ambao ni wahadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Laikipia.

Viongozi wa CHAKILA kwa sasa ni Bw Mwanza Mwaruwa (Mwenyekiti), Ann Mutemi (Naibu Mwenyekiti), Karisa Mwaduna (Katibu Mkuu), Ruth Kerubo (Katibu Msaidizi), Marion Wandera (Mhazini), Christabel Chebet (Afisa Mwenezi), Austin Konde (Katibu Mtendaji), Suleiman Mwarora (Afisa wa Mahusiano) na John David (Mhariri).

Wanachama huzuru shule mbalimbali za upili zilizoko karibu na Chuo Kikuu cha Laikipia ili kuwahamasisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa kukichapukia Kiswahili.

Mbali na kuhudhuria makongamano ya Kiswahili nje ya chuo chao, wanachama huandaa warsha ambapo wanafunzi wa shule mbalimbali za upili hualikwa ili kupalilia vipaji vyao katika sanaa mbalimbali.

Chama pia huandaa Siku ya Maadhimisho ya Vipawa ambapo wanachama hushiriki mashindano mbalimbali kwa nia ya kutononoa vipaji vyao katika sanaa za ulumbi, futuhi, utangazaji, uigizaji, uimbaji, usakataji densi na utunzi wa mashairi.

Mnamo 2018, wanachama hawa walichomoa filamu ya ‘Lost Dignity’ iliyoigizwa katika mashindano mbalimbali miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Afrika Mashariki.

Filamu hiyo iliwazolea tunu na sifa kedekede hasa baada ya maudhui yake kuangaziwa katika runinga ya NTV kama mojawapo ya kazi zinazoonyesha kwamba vijana wana uwezo wa kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa kiuchumi.

You can share this post!

Huenda Ruto akafukuzwa Jubilee Party

Kero ya stima kupotea bila notisi Zimmerman