• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Kero ya stima kupotea bila notisi Zimmerman

Kero ya stima kupotea bila notisi Zimmerman

Na SAMMY WAWERU

BAADHI ya wakazi wa mtaa wa Carwash, Zimmerman, Kaunti ya Nairobi wamelalamikia tabia za kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini, Kenya Power, kuwakatia stima mara kwa mara bila notisi.

Wakazi tuliozungumza nao wamesema kuwa wiki haikamiliki bila nguvu za umeme kupotea mara kadha.

“Imekuwa mazoea stima kupotea. Kinachoshangaza Kenya Power haitoi notisi,” akateta Denlaw Ken, mkazi.

Kijana huyu hufanya kazi ya kuandika na kutafsiri (academic writing), mwajiri wake akiwa ughaibuni.

“Ninapopewa majukumu, nichelewe kuwasilisha majibu hataelewa nguvu za umeme kupotea,” akasema, akilalamikia kuathirika pakubwa na kupotea kwa stima mara kwa mara eneo analoishi.

“Kazi ya uandishi ndiyo tegemeo langu kujiendeleza kimaisha na kulipa gharama ya bili Nairobi,” akasema.

Kabla kusitisha usambazaji wa nguvu za umeme katika eneo, Kenya Power hutoa notisi ya sehemu zitakazoathirika kwa kuchapisha kwenye magazeti na katika kurasa zake za mitandao, endapo inataka kuboresha huduma.

Mafundi wa Kenya Power wakifunga transfoma mpya katika mtaa wa Carwash, eneo la Zimmerman, Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Hitilafu inapotokea ghafla, hutoa tangazao katika kurasa zake za mitandao.

“Wapangaji wangu wamekuwa wakihangaika kupata maji kwa sababu hutumia nguvu za umeme kuyapampu kuweka akiba,” akasema keateka wa ploti moja eneo hilo.

Wakazi pia wanalalamikia shirika la Kenya Power kujikokota kuangazia hitilafu inapoibuka.

“Kutoka Carwash hadi Roysambu, ziliko afisi za Kenya Power, ni safari ya chini ya dakika 10 pekee, ila wanapoarifiwa hukawia kutuma mafundi,” akasema mkazi mwingine.

Mwezi uliopita, Agosti, kati ya tarehe 16 – 20, wenyeji walisalia gizani kufuatia kuharibika kwa transfoma.

Transfoma hiyo ililipuka na kuanza kumwaga mafuta, jambo ambalo ni hatari kwa wanaoishi katika mazingira yake.

“Tuna hitilafu inayotatiza eneo la kusambaza nguvu za umeme. Tafadhali tunaomba muda tuweze kuifuatilia,” kampuni hiyo ikaeleza kupitia ujumbe, siku kadha baada ya kuarifiwa.

Aidha, ilichukua muda wakazi kurejeshewa stima.

Kampuni hiyo ilibadilisha transfoma iliyokuwa na hitilafu, kwa kuweka nyingine.

Baadhi ya wakazi walidai tatizo hilo lilitokana na utepetevu wa Kenya Power, mafundi wake walipokuwa wakifanya rekebisho mnamo Agosti 16, 2021.

You can share this post!

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili chuoni Laikipia ni...

Farouk Shikhalo asajiliwa na KMC ya Tanzania