• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:50 AM
Wakuzaji maua ya Arabicum walia hasara ya ‘soft rot’

Wakuzaji maua ya Arabicum walia hasara ya ‘soft rot’

NA PETER CHANGTOEK

WAKULIMA wanaokuza maua aina ya Arabicum, wanalilia usaidizi kwa sababu ya ugonjwa unaothiri mimea yao.

Ugonjwa huo, unaojulikana kama ‘bulb rot’ ama ‘soft rot’, huathiri mizizi ya mmea huo, ambapo huoza na hatimaye mmea hukauka na kuanguka.

Maua yamekuwa yakiiletea nchi kiwango kikubwa cha fedha kutoka ughaibuni, na sasa wakulima hao wanahofia fedha hizo huenda zikakosa kuingia nchini, endapo ugonjwa huo hautadhibitiwa.

Kwa mujibu wa Richard Matheri, mwenyekiti wa State Lodge Self Help Group – kundi la wakulima wanaokuza maua katika eneo la Sagana, Kaunti ya Nyeri, ugonjwa huo unatishia kuangamiza mimea yao kabisa.

“Kila mkulima anayekuza maua anapitia changamoto ya ugonjwa huo. Tumejaribu kemikali kadhaa. Sisi huuzia kampuni ya Wilmar Flowers, ambayo imekuwa ikituletea dawa,” asema mkulima huyo, ambaye amekuwa akikuza maua kwa muda wa zaidi ya miaka 20.

Matheri, ambaye ni mmojawapo wa wakulima wa kwanza kuanza kuyakuza maua katika eneo hilo, anasema kuwa, hiyo ndiyo changamoto kuu mno kwao.

Rachel Kagendo pia ni anakuza maua hayo na ni miongoni mwa walioathiriwa. Yeye hulitumia shamba nusu ekari kwa shughuli za kilimo.

“Nimekuwa nikikuza maua kwa muda wa miaka minne. Ugonjwa huo umekuwepo na unatishia kuangamiza mimea. Tumejaribu kutumia kemikali tofauti tofauti lakini hatujafanikiwa,” asema Kagendo.

Anaongeza kwamba, akilinganisha faida anayopata kutoka kwa maua na ile anayopata kutoka kwa mimea mingine, maua ndiyo humpa fedha nyingi.

“Tukipata kemikali, itakuwa vizuri kwa sababu ni kilimo-biashara kilicho na faida,” adokeza.

Lydia Mureithi, ambaye ni mwanachama wa State Lodge Self Help Group, anasema kwamba mimea yake imeathirika pia.

“Niliacha kukuza kwa muda wa miaka sita. Nilianza kukuza tena 2021. Hakuna tiba; tumetumia dawa nyingi lakini hatujafanikiwa,” asema mkulima huyo.

Anadokeza kuwa, alikuwa akitarajia kuvuna mashina 8,500 baada ya kupanda mbegu magunia matano katika shamba lake la robo ekari lakini hakufaulu.

Kwa mujibu wa Carol Mutua, mtaalamu wa uzalishaji wa mimea katika Chuo Kikuu cha Egerton, ni kuwa, ugonjwa huo wa ‘soft rot’ husababishwa na bakteria aina ya Erwinia carotovora.

Mtaalamu huyo anaongeza kuwa, mimea inayoathiriwa na ugonjwa huo, hutoa harufu kali na mbaya kutoka kwa mizizi.

Bw Ngatia akionyesha mimea iliyoathiriwa na ugonjwa. PICHA | PETER CHANGTOEK

Anashauri kuwa, ili kuzuia ugonjwa huo, wakulima wanafaa kuzikuza mbegu safi, ambazo hazijaathiriwa na ugonjwa.

Anasema kuwa, wanapopalilia mimea, wakulima wanafaa kuwa waangalifu wasije wakadhuru mizizi akiongeza kuwa mbegu zinafaa kuwekwa kwa kemikali aina ya ‘copper’, ili kuua bakteria.

“Majani hubadili rangi na kuwa na rangi nyeusi. Ugonjwa huo umeenea katika kaunti tofauti tofauti,” anaeleza David Mwoya, mwanaagronomia kutoka kampuni ya Wilmar Flowers.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Rais Uhuru na Ruto wakomeshe tofauti zao za...

CECIL ODONGO: Madai ya Ruto kumsaidia Uhuru kushinda kura...

T L