• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
WANGARI: Mageuzi katika sekta ya kilimo yazingatie pia usalama wa raia

WANGARI: Mageuzi katika sekta ya kilimo yazingatie pia usalama wa raia

Na MARY WANGARI

MISWADA kadhaa imepitishwa ili kufanyia mageuzi sekta ya kilimo na kuboresha maslahi ya wakulima ambao wamehangaika kwa miaka mingi.

Waunda sheria wamejitokeza kuwatetea wakulima dhidi ya ushindani usio wa haki kutokana na wingi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa ya kigeni ambazo huuzwa kwa bei duni.

Mabadiliko hayo yatafaidi maelfu ya wakulima ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilia kuhusu hasara wanayopata kutokana na kufurika kwa bidhaa kutoka nchi za kigeni, zinazouzwa kwa bei ya chini.

Kuanzia samaki, mayai, sukari, vitunguu na kadhalika, masoko na maduka ya jumla nchini yamekuwa yakijazwa bidhaa zinazoagiziwa kutoka mataifa jirani na kuwaacha wakulima nchini wakiwa hoi.

Uimarishaji wa kilimo utachangia kuunda nafasi za ajira na kuimarisha viwanda jambo litakalowafaa maelfu ya vijana ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa ajira.

Hii ni hatua muhimu ikizingatiwa ni mojawapo wa Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu uongezaji thamani kwa bidhaa za kilimo.

Japo juhudi hizo zinapaswa kupongezwa kwa kupatia kipaumbele maslahi ya raia, si jambo la kushangaza kwamba wabunge na wanasiasa wanaonekana ghafla kuanza kupatia kipaumbele maslahi ya raia.

Hii ni kwa kuzingatia kuwa msimu wa kampeni unakaribia kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Katika juhudi za kutaka kuvutia wapiga kura ili wapate kuchaguliwa tena, wanasiasa hujitahidi kwa kila hali ikiwemo kuungana na kupitisha sheria ambazo huwafaidi wananchi na wakati mwingine kuwaathiri.

Hata hivyo, maamuzi hayo yanapofanywa kiholela kwa minajili tu ya kuvutia wapiga kura, baadhi ya sheria hizo huishia kuwaumiza wateja na uchumi wa nchi kwa jumla.

Mfano mzuri ni kuhusu Mswada wa Fedha 2021 ambao unahusu masuala mengi ya mwananchi wa kawaida kuanzia bidhaa kama vile pikipiki na shughuli za kilimo.

Kwa kuidhinisha sheria kuhusu kutozwa ushuru wa asilimia 16 wa VAT ikiwemo ada nyinginezo dhidi ya bidhaa za kigeni zinazoagizwa nchini, ni wazi kwamba bei ya bidhaa hizo itapanda na raia wengi hawataweza kuimudu.

Isitoshe, hatua ya kuzuia ushindani kwa kufungia nje bidhaa za kigeni, pana tishio la wakulima na wenye viwanda nchini kulegeza kamba kuhusu viwango vya ubora na kuzalisha bidhaa duni.

Hii ni kwa sababu wana hakika ya kupata soko bidhaa zao ziwe bora au vinginevyo hivyo, baadhi hawatajishughulisha mno na mwishowe, ni wateja tu watakaoumia kwa kukosa bidhaa bora.

Ingawa juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo zinafanywa kwa nia njema, ni sharti kuwe na tahadhari zisije zikaleta madhara zaidi kuliko manufaa.

[email protected]

You can share this post!

TSC yafungua roho kwa Knut baada ya Sossion kuondoka

ODONGO: Wanaopinga Ruto wauze sera kujifaa kisiasa nchini