• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
ODONGO: Wanaopinga Ruto wauze sera kujifaa kisiasa nchini

ODONGO: Wanaopinga Ruto wauze sera kujifaa kisiasa nchini

Na CECIL ODONGO

MATAMSHI ya Gavana wa Kitui Charity Ngilu kuwa upinzani unafaa uungane kwa lengo la kumzuia Naibu Rais Dkt William Ruto kutwaa kiti cha Urais, hayatawasaidia kisiasa.

Inasikitisha kuwa mwanasiasa mwenye uzoefu kama yeye anaweza kutoa kauli kama hiyo kwani matarajio ya wengi ni kuwa atakuwa katika mstari wa mbele kusisitizia umoja wa nchi na uwajibikaji kwa raia.

Kauli ya Bi Ngilu inarejesha kumbukumbu za kihistoria hasa wakati wa kupigania mfumo wa vyama vingi miaka ya 90 ambapo upinzani uliungana pamoja kwa minajili ya kumwondoa aliyekuwa Rais Daniel Arap Moi mamlakani.

Mnamo 1991 kigogo wa siasa za upinzani marehemu Jaramogi Oginga Odinga pamoja na Masinde Muliro, Kenneth Matiba, Martin Shikuku, Gitobu Imanyara, Raila Odinga waliunda chama cha Ford kwa lengo tu la kutamatisha uongozi wa Kanu na kumwondoa Mzee Moi uongozini.

Hata hivyo, kutokana na tamaa yao ya uongozi, muungano wao uligawanyika na kukaibuka vyama vya Ford Kenya na Ford Asili.

Mwishowe, Mabw Matiba na Oginga walienda njia zao na kupoteza kura kwenye uchaguzi wa 1992 kwa Kanu.

Huenda kauli ya Bi Ngilu ilichochewa na tukio hilo la uchaguzi wa 1992 ambapo upinzani ulishindwa kutokana na mgawanyiko uliokuwepo wakati huo.

Pia usemi wa Bi Ngilu huenda ulisukumwa na ushindi wa Mwai Kibaki mnamo 2002 uliomaliza utawala wa karibu miaka 40 wa Kanu.

Wakati huo upinzani uliungana ndani ya Muungano wa Narc na Bw Kibaki akafanikiwa kumbwaga Uhuru Kenyatta wa Kanu uchaguzini.

Baadhi ya vyama vilivyobuni Narc ni DP ya Kibaki, Ford Kenya ya Wamalwa Kijana na

SDP ya Bi Ngilu. Watatu hao waliungana

chini ya NAK ambayo ilibadilika ikawa Narc baada ya kujumuishwa kwa LDP ya Mabw Odinga, Musyoka na Mzee Moody Awuori.

Hata hivyo, wakati huu siasa zimebadilika na kukiri kwa Bi Ngilu kuwa upinzani uungane ni dhihirisho tosha kwamba Naibu Rais anajivunia umaarufu mkubwa nchini na yupo katika nafasi nzuri ya kuingia Ikuluni.

Kinaya ni kwamba wanaotakiwa waungane tayari kila moja wao amesema atawania urais mwakani wala hawawezi kulegeza kamba kwa kuwa wamemuunga mkono Bw Odinga tangu 2013.

Iwapo kila mmoja wao atachukua mkondo tofauti wa kisiasa basi kuna uwezekano mkubwa Dkt Ruto atatamba 2022.

Duru zinaarifu kwamba baadhi ya vinara hao wapo radhi kuingia kambi ya Dkt Ruto hali inayoifanya iwe vigumu zaidi kwa muungano anaoupigania Bi Ngilu kuafikiwa.

Aidha, badala ya kujikita katika kampeni za kumzuia Dkt Ruto kuingia mamlakani, vinara wa Nasa wanafaa waeleze raia sera zao ili raia waamue mustakabali wao wa kisiasa.

Pia wafahamu kuwa Naibu Rais ni mwanasiasa mkakamavu ambaye anajipanga na kunadi sera zake akilenga ikulu.

Dkt Ruto tayari anajivunia uungwaji mkono kutoka maeneo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya ambayo yana wapigakura wengi zaidi nchini.

Wanasiasa kama Bi Ngilu wafahamu kuwa kuungana kwa ajili ya kumzuia mtu mmoja kuingia mamlakani kunaweza kusababisha chuki na ghasia jinsi ilivyokuwa mnamo 2007.

[email protected]

You can share this post!

WANGARI: Mageuzi katika sekta ya kilimo yazingatie pia...

SHINA LA UHAI: Nimonia: Nduli anayewaandama watoto kila...