• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
WASONGA: Bandari: Serikali itimize ahadi kwa wakazi Lamu

WASONGA: Bandari: Serikali itimize ahadi kwa wakazi Lamu

Na CHARLES WASONGA

ALHAMISI Rais Uhuru Kenyatta alizindua rasmi bandari mpya ya kisasa ya Lamu ambayo ni hatua ya kwanza katika utekelezaji wa mradi wa uchukuzi kati ya Lamu, Sudan Kusini na Ethiopia (Lapsset).

Bila shaka mradi huu, ambao ni sehemu ya miradi mikuu chini ya mwavuli wa Ruwaza ya Maendeleo ya 2030, utachochea biashara ya uchukuzi wa bidhaa kati ya Kenya na nchi za Sudan Kusini na Ethiopia ambayo ni hatua itakayozalisha nafasi za ajira na kupiga jeki biashara katika Kaunti ya Lamu.

Hii ni kwa sababu bandari hii itapokea meli kubwa, sawa na ile ambayo Rais Kenyatta alipokea jana, ambayo huhudumu katika Bahari Hindi, Bahari ya Shamu na ile ya Mediterrenean. Bandari hii pia itachangia ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta, reli ya kisasa na ujenzi wa miji kadha katika kaunti za Isiolo na Turkana.

Chini ya kivuli hiki, Serikali ya Kitaifa inafaa kusikia kilio cha viongozi wa Kaunti ya Lamu kwamba wakazi wa eneo hilo wapewe kipaumbele katika ajira. Nakubaliana na mantiki ya viongozi wa eneo hilo, wakiongozwa na Gavana Fahim Twaha, wakazi, haswa vijana wapewe ajira katika bandari hiyo.

Ni kawaida kwamba mradi wote unapoanzishwa mahala fulani nchini Kenya, huibua matumaini makubwa kwa wakazi wa eneo husika wakitarajia kupata ajira na nafasi za kibiashara. Isitoshe, hata Sheria ya Serikali za Kaunti kuhusu ajira inasema kuwa asilimia 70 ya nafasi za ajira katika kaunti zinapaswa kuwaendea wakazi huku asilimia 30 zikijazwa na watu kutoka sehemu zingine za nchi.

Lakini inavunja moyo kwamba Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) na serikali kuu, hazionekani kuheshimu kanuni hiyo na hivyo kuchangia lalama kutoka kwa viongozi na wakazi wa Lamu.

Kwa mfano, tayari KPA inaonekana kuvunja ahadi aliyotoa Rais mstaafu Mwai Kibaki mnamo 2012 alipozindua mradi wa Lapsset kwamba jumla ya wanafunzi 1,000 wapewe udhamini wa mafunzo yatakayowawezesha kuajiriwa katika bandari ya Lamu.

Hii ni kwa sababu, kulingana na viongozi wa Lamu, ni wanafunzi 400 pekee wamedhaminiwa kufanya kozi mbalimbali zinazohusu elimu ya majini chini ya mpango huo unaofahamika kama “Lapsset Presidential Scholarship Scheme”.

Serikali inapaswa kutoa mwelekeo na mwongozo wa kusajiliwa kwa wanafunzi 600 waliosalia chini ya mpango huu ili wakazi wa Lamu wahisi kutendewa haki.

Lakini kwa upande mwingine, viongozi wa kisiasa wanaosuta KPA kwamba inabagua wakazi wa Lamu katika ajira wanafaa kuanika hatua ambazo wamechukua kuwaandaa vijana kuajiriwa katika bandari ya Lamu.

Ikizingatiwa kuwa ujenzi wa bandari hii ulianza mwaka wa 2012, nadhani kufikia sasa wanasiasa wa Lamu wangekuwa wameanzisha wakfu wa kutoa udhamini wa mafunzo kwa vijana ili waweze kupata ajira katika mradi huo.

Kwa mfano, badala ya Gavana Twaha na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Lamu Ruweidha Obbo kulalamika, waseme hatua ambazo wamachukua kufadhili mafunzo kwa vijana ili kuwaandaa kwa nafasi za ajira katika bandari mpya ya Lamu.

Kama shirika la Serikali Kuu, KPA haiwezi kuajiri mtu yeyote asiye na ujuzi hitajika kwa sababu yeye ni mwenyeji wa Lamu.

Kwa hivyo, sharti viongozi watumie rasilimali za afisi zao kuwadhamini vijana wengi ili waweze kuajiriwa katika mradi huo. Watakaokosa kazi hawafai kuvunjika moyo kwani bado wanaweza kufaidi kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo karibu na bandari hiyo mpya.

You can share this post!

Colombia yapoteza fursa ya kuandaa fainali za Copa America...

MATHEKA: BBI: Viongozi wakome kuchochea umma dhidi ya majaji