• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Colombia yapoteza fursa ya kuandaa fainali za Copa America 2021

Colombia yapoteza fursa ya kuandaa fainali za Copa America 2021

Na MASHIRIKA

COLOMBIA hawatakuwa tena waandalizi wenza wa Argentina wa fainali za Copa America 2021 baada ya ongezeko la msururu wa visa vya maandamano nchini humo.

Kipute hicho cha Copa America kilikuwa kimeratibiwa kuandaliwa kwa pamoja na Colombia na Argentina na hiyo ingekuwa kwa mara ya kwanza tangu 1916 kwa fainali hizo kuandaliwa na mataifa mawili

Kumeshuhudiwa visa vingi vya maandamano nchini Colombia ambapo wananchi wamekuwa wakilalamikia matukio ya unyanyasaji kutoka kwa serikali ambayo iliongeza ushuru kwa bidhaa muhimu na za msingi mnamo Aprili 2021.

Matukio hayo yamevuruga pia baadhi ya michuano ya Copa Libertadores – kipute ambacho hadhi yake ni sawa na mashindano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA).

Fainali za Copa America ambazo huleta pamoja jumla ya vikosi 10 zilikuwa zimeratibiwa kufanyika kati ya Juni 13 na Julai 10 jijini Barranquilla.

Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) limefikia maamuzi ya kuondoa fainali hizo za Copa America nchini Colombia baada ya kufutilia mbali ombi la taifa hilo kwa mashindano hayo kuhamishwa hadi Novemba 2021.

Argentina sasa watasalia kuwa wenyeji wa pekee wa fainali hizo za Copa America huku baadhi ya michuano ya kimataifa iliyokuwa ifanyike Colombia ikihamishwa hadi Paraguay na Ecuador kwa sababu ya maandamano hayo na pia ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini Colombia.

Hadi kufikia Mei 20, 2021, zaidi ya vifo 83,000 kutokana na corona vilikuwa vimeripotiwa nchini Colombia. Argentina imeweka kanuni kali za kudhibiti maambukizi ya corona na inapania kutolegeza baadhi ya msharti hayo hadi Mei 31, 2021.

Brazil ndio mabingwa watetezi wa taji la Copa Amerika.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Yafaa Rais aupime ushauri anaopewa

WASONGA: Bandari: Serikali itimize ahadi kwa wakazi Lamu