• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
ZARAA: Mwalimu avuna faida za kuzamia kilimo

ZARAA: Mwalimu avuna faida za kuzamia kilimo

NA PETER CHANGTOEK

KATIKA shamba la ekari saba na nusu katika eneo la Muani, kilomita tano kutoka Sultan Hamud, ukielekea Kasikeu, mkulima mmoja anachangamkia zaraa ya ukuzaji wa mimea ya aina tofauti.

Patrick Mutiso, 46, anayefunza katika Shule ya Upili ya Mutulani, amekuwa akiendeleza ukuzaji wa mimea ya mipapai, nyanya, pilipili mboga, mitikiti na mihindi miongoni mwa mimea mingine.

Alianza kutilia maanani shughuli za ukulima wakati wa ugonjwa wa Covid-19.

“Nilianza kwa kuikuza mipapai kwa sababu sikuwa na maji lakini jirani yangu alikuwa na maji na akanisaidia ya kunyunyizia. Nilianza kwa kuikuza mipapai 240,” asema Mutiso.

Wakati anapoipanda mipapai, huacha nafasi ya mita tatu kutoka kwa mmea mmoja hadi mwingine.

Huikuza mipapai aina ya Solo Sunrise anayosema huchukua muda wa miezi sita. Pia hukuza aina nyinge za mipapai.

Mutiso, ambaye hutumia mbolea asilia ya mifugo kuikuza mimea yake, anadokeza kwamba alinunua miche katika eneo la Salama kwa Sh70 kila mmoja.

Hata hivyo, miche kadhaa iliangamizwa na kiangazi, lakini hakufa moyo.

Anasema kuwa, mojawapo ya changamoto anazopitia katika ukuzaji wa mipapai ni wadudu aina ya whiteflies wanaovamia mimea.

Ili kuwakabili, hushurutika kunyunyizia dawa.

Ndege wanaoyavamia matunda shambani pia ni changamoto, japo si changamoto ya kumpa wasiwasi mwingi.

Huyauza matunda yake kwa wateja wanaoenda kununua shambani, hususan marafiki na wateja wengine. Huliuza papai moja kwa kati ya Sh50 na Sh150.

“Huwa napenda kuuza moja moja na si kuuza kwa kilo,” asema, akiongeza kuwa, tunda moja linaweza kuwa na kilo moja na nusu.

Mbali na mipapai, mkulima huyu huikuza mimea ya nyanya aina ya Big Rock F1, katika sehemu moja ya shamba lake.Pia, Mutiso huikuza mimea ya pilipili mboga katika sehemu nyingine ya shamba hilo. Anasema kwamba wateja wa pilipili mboga hutoka maeneo ya Mlolongo na Nairobi.

“Pilipili mboga zina soko. Nilipokuwa nikianza kilo moja ilikuwa ikiuzwa kwa Sh45, lakini imepanda hadi Sh90,” asema.

Anafichua kuwa, baada ya 2020 ndipo alipoanza kuikuza mimea ya pilipili mboga, na akagundua kuwa ina faida. Anasema kuwa huchuma kilo 1,000 kwa wiki katika shamba ambalo halifiki ekari mbili.

“Pilipili hoho haziathiriki sana na magonjwa. Changamoto kubwa ni wakati wa baridi; kati ya Juni na Julai,” asema, akiongeza kuwa, usafi ni muhimu shambani.

Mkulima huyo, pia huikuza mitikiti na anafichua kwamba, wiki chache zilizopita, alivuna tani 30 za matikitimaji ambapo aliwauzia wateja kutoka Nairobi.

Kadhalika, anaeleza kuwa alifaulu kuchimba kisima mnamo mwezi Juni ili kupata maji ya kutumia shambani kuikuza mimea.

  • Tags

You can share this post!

MITAMBO: Ni afueni mfumo wa kuunda bayogesi ukikata gharama

Tshisekedi asutwa kuingiza wageni mgogoro wa DRC

T L