• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
MITAMBO: Ni afueni mfumo wa kuunda bayogesi ukikata gharama

MITAMBO: Ni afueni mfumo wa kuunda bayogesi ukikata gharama

NA RICHARD MAOSI

MATUMIZI ya bayogesi ni njia mojawapo ya vyanzo vya nishati kwa manufaa mbalimbali ya nyumbani.

Gesi hii hutengenezwa kutokana na mabaki ya viasilia katika mazingira yasiyokuwepo na oksijeni.

Akilimali ilipata fursa ya kutembelea Sams Farm Lanet ambapo tulikumbana na mkulima ambaye amefaidi matumizi ya bayogesi ambayo mara nyingi hutengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea kama vile ya miwa, mikonge na samadi.

Gambi Gitonga ni mkazi wa eneo la Kiamunyeki, Lanet katika barabara ya Nakuru kuelekea Olkalou.

Kiamunyeki ni sehemu ambayo hupokea mvua ya kadri, jambo ambalo limewasukuma wakazi hapa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, nguruwe, mbuzi na kondoo.

Katika kipande cha ardhi cha ekari 21, Gitonga ni mfugaji wa ng’ombe 80 wa maziwa, nguruwe 300, vilevile anakuza mahindi na nyasi za mifugo almaarufu kama boma grass.

Kulingana na Gitonga, kukuza lishe hufanya gharama ya ufugaji kuwa nafuu, ambapo hununua tu malighafi kama vile canola kuongezea virutubisho kwenye lishe ya mifugo yake.

Awali alikuwa akitumia samadi kama mbolea shambani mwake, lakini kadri idadi ya mifugo ilipozidi kuongezeka hali ikageuka na kuwa kero kwake kutokana na harufu kali na uvundo, hususan inayotokana na samadi.

Safari yake

Mwanzoni mwa 2018 Gitonga akaanza kufanya utafiti na kugundua kwamba inawezekana kuzalisha mbolea, nishati ya kawi safi na gesi (bayogesi).

Aliamua kutumia akiba yake kununua mtambo wa kisasa wa bio-digestor ambao una uwezo wa kuendesha shughuli zote za shambani kama vile kuendesha jenereta, mashine ya kukama, na kuwasha majokofu ya kuhifadhi maziwa na nyama shambani.

“Niligundua sihitaji tena kukata miti na ninawashauri wakulima wanaofuga nguruwe, ng’ombe na hata punda kukumbatia matumizi ya bayogesi badala ya kutegemea makaa au kulipia stima,” asema.

Anasema mara tu baada ya kukusanya samadi kutoka shambani, hubebwa na kuingizwa ndani ya chemba maalum ya bio -digestor.

Gamba Gitonga (kulia) mkazi wa Kiamunyeki barabara ya Lanet-OlKalou akionyesha mtambo wa kisasa wa bio-digestor ambao hutumika kuchakachua mabaki ya viasilia kutengeneza gesi ya bayogesi ambayo hutumika kwa matumizi mbalimbali ya shambani. PICHA | RICHARD MAOSI

Katika mchanganyiko huo ndoo tatu za maji huongezwa katika kila ndoo ya samadi kisha akachanganya vyema mseto wa maji na samadi na kutengeneza kitu kiowevu ambacho huzalisha mvuke wa gesi.

Gesi hii huelekezwa katika sehemu mbalimbali za shamba kupitia paipu ambazo hutokea katika mabomba maalum ya kuhifadhi gesi.

Gitonga anasema tangu aanze kujitengenezea gesi amefanikiwa kupunguza gharama ya kulipia stima kutoka Sh40,000 kila mwezi hadi Sh18,000 kila mwezi.

“Pili, matumizi ya bayogesi yamekuwa yakinisaidia kupunguza kero ya ukataji miti kiholela ikilinganishwa na zamani wakati ambapo wafanyikazi walikuwa wakitumia kuni kupikia,” asema.

Aidha, Gitonga anasema anaweza kupata mbolea safi ambayo hutumika kukuza mahindi na nyasi aina ya boma ambayo hutumika kulisha mifugo.

Pia anawashauri wakulima kujifunza mbinu mbalimbali za kuendesha kilimo kwa kuzingatia mfumo wa uzalishaji kawi safi ili kutunza mazingira na kwa wakati huo kukumbatia mifumo ya kupunguza gharama za matumizi shambani.

Pili, anawahimiza wakulima kukumbatia teknolojia za kisasa ambazo zitawasaidia kutengeneza faida ya haraka na kuongeza thamani katika kilimo.

  • Tags

You can share this post!

NJENJE: Afueni kwa wafugaji serikali ikitangaza kuondoa...

ZARAA: Mwalimu avuna faida za kuzamia kilimo

T L