• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
BENSON MATHEKA: Ili kuadhibu viongozi wabaya, vijana wajisajili kupiga kura

BENSON MATHEKA: Ili kuadhibu viongozi wabaya, vijana wajisajili kupiga kura

Na BENSON MATHEKA

KUNA kila dalili kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)) haitatimiza lengo lake la kusajili wapigakura wapya 4.5 milioni katika zoezi linaloendelea.

Tume hiyo ililenga idadi hiyo katika zoezi la mwezi mmoja linalokamilika siku tano zijazo.Kufikia Jumanne wiki hii, tume ilikuwa imesajili wapigakura 800,000. Ishara kwamba haingetimiza lengo lake zilionekana vijana ambao ndio wanaolengwa walipodai kwamba hawaoni sababu ya kupiga kura kuchagua viongozi wasiowasaidia.

Vijana kote nchini wanalalamika kuwa hakuna kiongozi wanayechagua anayetimiza ahadi anazotoa wakati wa kampeni.Huu ni ukweli mtupu lakini sio sababu ya kutosha kukataa kujisajili kuwa mpigakura kwa kuwa ni kwa kupiga kura ambapo wanaweza kuchagua viongozi wanaoweza kubadilisha uongozi.

Japo ni kweli viongozi wamekuwa wakiwasahau wapigakura wanapoingia uongozini na kuweka sera na maamuzi yanayofanya maisha ya raia kuwa magumu zaidi ukiwemo wizi wa pesa za umma, kususia kujisajili kupiga kura na kwa kukosa kupiga kura kunatokana na uelewa finyu wa haki za demokrasia. IEBC inafaa kukubali kuwa haikutoa elimu ya jamii ya kutosha kuhamasisha vijana umuhimu wa kupiga kura.

Elimu ya jamii ni muhimu kabla ya zoezi la kusajili kura kuanza.Ni makosa kwa tume kuamini kuwa vijana wapatao milioni tano waliopata vitambulisho vya kitaifa tangu 2017 wanafahamu haki zao na umuhimu wa kupiga kura wakati ambao wanapambana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na maamuzi ya viongozi waliochaguliwa.

Viongozi wenyewe wanafahamu hayo na ndio sababu wito wao kwa vijana kujitokeza kusajiliwa kuwa wapigakura umepuuzwa na vijana 4.1 milioni waliolengwa katika zoezi linaloendelea.Kwa kuwa IEBC imesema kuwa haitaongeza muda wa kusajili wapigakura wapya ukikamilika siku tano zijazo na ikizingatiwa kuwa Wakenya wengi wanaonekana kukosa imani na uchaguzi mkuu, kuna uwezekano mkubwa kwamba watu wasiojali maisha ya raia watarudi uongozini baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Ili kuepuka hali kama hii, vijana, ambao ndio wanaoathiriwa zaidi na uongozi mbaya hawana budi kubadilisha nia na kujitokeza kwa wingi kujisajili kupiga kura. Wakikosa kufanya hivyo hawatakuwa wakiadhibu IEBC kwa kuwa haina cha kupoteza bali wanajiadhibu wenyewe na nchi yao.

Ni kwa kujisajili kupiga kura na kujitokeza kupiga kura ambapo raia wanaweza kuadhibu viongozi wabaya kwa kukosa kuwachagua. Demokrasia hufaidi raia wanaoishiriki kikamilifu sio wanaopuuza haki na majukumu yao.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: IEBC yafaa kulaumiwa kwa idadi ndogo ya...

Makueni yapinga agizo Taveta itoze kodi Mtito

T L