• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Chunga usiwe ‘mzazi hewa’ kwenye maisha ya mwanao

Chunga usiwe ‘mzazi hewa’ kwenye maisha ya mwanao

NA WINNIE ONYANDO

WAZAZI wengi leo hii wametelekeza majukumu yao ya kuwaangalia na kuwalea watoto wao kwa njia ya uadilifu, kisingizio kikiwa ni kubanwa na shughuli za kikazi.

Wanatafuta pesa na kusahau umuhimu wa kupalilia husiano wa karibu na watoto wao.

Kutafuta pesa si jambo baya, lakini ni muhimu kuelewa kuwa uwepo wa mzazi katika maisha ya mtoto ni muhimu na una athari kubwa katika ujenzi wa tabia, mienendo yake, na kwa njia moja au nyingine, alama anazopata kwenye masomo shuleni.

Ripoti ya 2019 iliyochapishwa na ‘Transform Nations’ chini ya mpango wa ‘Man Enough’ ilionyesha kuwa, asilimia 45 ya watoto nchini wanaishi na mzazi mmoja au hawana kabisa.

Watoto wanapokua, wanahitaji matunzo na umakinifu wa kutosha kutoka kwa wazazi wao.

Uhusiano kati ya mzazi na mwanawe unaweza kudidimia sana kipindi mzazi anakuwa mbali na mwanawe, na hii inaweza kumwathiri kwa kiasi kikubwa kama walivyoainisha Mwoma & Pillay (2015).

Kwa kiasi kikubwa, mama mzazi, kama mlezi, mara nyingi huwa karibu zaidi na mwanawe, akimpa muda na tahadhari pale inapostahili.

Hali ni tofauti kiasi kwa wazazi wa kiume ambao mara nyingi mbali na kazi, baadhi yao huweka mbele starehe kama vile kutazama mpira kwa runinga kwenye vilabu.

Mara nyingi wao hurudi nyumbani majira ya usiku.

Utafiti uliofanywa na Allen na Daly (2007) nchini Amerika ulionyesha kuwa, baadhi ya watoto ambao wanalelewa na mama pekee bila uwepo wa baba huwa na athari za kisaikolojia kwa mfano unyogofu, fikra za kujitia kitanzi na matumizi ya dawa za kulevya.

Kwa hivyo, muda wa starehe ni muhimu, lakini ni bora kwa mzazi wa aina hiyo kutafuta namna atawahusisha wanawe kipindi ambacho hawako shuleni, huku akiwapa mawaidha.

Ni jukumu la kila mzazi kutenga muda wa kutosha kuwa karibu na mtoto, hata ikiwa unafanya kazi inayohitaji umakini kiasi gani.

Kadhalika, usimwache mtoto wako alelewe na mjakazi tu saa zote. Kazi isiwe kikwazo kati yako na mwanao, na afya yake ni muhimu zaidi kuliko pesa unazotafuta.

Ni kawaida siku hizi wazazi wengi kuwatelekeza watoto wao na kuzamia majukumu yanayolenga kuwatajirisha bila kujali kwamba, huenda watoto hao wakaathirika pakubwa kimawazo, hasa wakati wanakua.

Hali hii hasa inajidhihirisha zaidi miongoni mwa wazazi wa kiume ambao hawafuatilii kwa karibu ukuaji wa watoto wao.

Wengine hata hawafuatilii hali ya masomo ya watoto hao na baadhi hushtukia wanapogundua baadaye kwamba watoto hao hawafanyi vyema shuleni.

Wengine vile vile hushangaa wanapofahamishwa baadaye kwamba, wanao ama ni wahalifu au ni waraibu wa vileo hatari.

Mbali na uwepo wako, mtoto anahitaji kujengwa kifikra na kuhakikishiwa kuwa ni mrembo au mtanashati.

Kuonyesha upendo, kutoa pongezi, na kushughulikia afya yake ni sehemu muhimu ya malezi.

Uwepo wa mzazi unachochea motisha, ujasiri, na nguvu ndani ya mtoto. Hutoa msingi wa utulivu wa kihisia, furaha, na amani moyoni mwake.

Jitahidi kukaa karibu na mwanao. Keti chini naye, zungumza, na mfahamu vizuri.

Hii itakusaidia kujua mawazo yake, hofu, nguvu zake, na mahitaji yake ya kibinafsi.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Michael Warutere: Mtahiniwa aliyezoa alama 428 katika KCPE...

Garissa, Kwale zilikuwa na watahiniwa wengi walio na umri...

T L