• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
JURGEN NAMBEKA: Watoto walindwe na haki zao kuzingatiwa msimu huu

JURGEN NAMBEKA: Watoto walindwe na haki zao kuzingatiwa msimu huu

NA JURGEN NAMBEKA

TUKIO la hivi majuzi la wahuni kumnyofoa macho mtoto wa umri wa miaka mitatu katika eneo la Kisii, limewaacha wazazi wengi na wasiwasi kuhusiana na wanayeweza kuwaachia wana wao.

Cha kusikitisha ni kuwa, washukiwa wakuu katika kisa hicho cha uhaini, ni wale wanaodaiwa kuwa karibu sana na mtoto huyo.

Tukio hilo limeibua hofu kuhusiana na usalama wa watoto hasa katika msimu huu wa Sikukuu ya Krismasi.

Wazazi wengi nchini wamepanga safari za kuelelekea sehemu mbalimbali, ili kujivinjari.

Wengi wao wamepanga likizo hiyo kwa ajili ya kuwa na muda mzuri wa kutangamana na wanao.

Licha ya polisi na taasisi nyingine za usalama kutangaza kuwa zimeongeza juhudi za kiusalama, haitoshi kuhakikisha kuwa kila mmoja atakuwa salama wakati huu wa sherehe za Krismasi.

Ni wazi kuwa wazazi watalazimika kumakinika zaidi hata wanapofika katika maeneo ya kujivinjari.

Mara nyingi wahuni kama vile watekaji nyara, hutumia sehemu zenye watu wengi kutekeleza uhalifu wao.Kwa hivyo ni vyema iwapo wazazi watajiandaa kusherehekea Krismasi katika sehemu za wazi za kujivinjari, ila kwa kutahadhari.

Iwapo mzazi atakuwa katika mazingira mapya, basi awe macho na kufuatilia anachofanya mwanae.

Wazazi wanaozuru fukwe za bahari ama vidimbwi wanafaa pia kutahadhari ili watoto wasijipate kwenye hatari. Ikiwa kwa mfano mtoto hajui kuogelea, basi vyema kuhakikisha kuwa haingii kwenye ina kirefu.

Ni muhimu pia kuwa na utaratibu wa kukabili hali ya hatari kabla ya kuelekea sehemu uliyopanga kujivinjari.

Kwa mfano, iwapo kuna watoto wengi, mzazi anaweza kumpa mwanawe sehemu maalum ya kukutana naye, endapo atapotea.

Ni muhimu hata hivyo katika hali zote kuhakikisha usalama wa watoto na kuwaepushia hatari za aina yoyote.

Hata hivyo, wengi wanapoendelea kulaani unyama aliotendewa mtoto Sagini, kisa hicho pia ni wito kwa wazazi kuwa makini zaidi na maisha ya wana wao pamoja na mazingira wanamoishi.

Iwapo waliokaribu na wanao wanaweza kutekeleza unyama kama ule, ni muhimu kwa wazazi kuwa makini. Ni ukumbusho kuwa wazazi wanapaswa kuwa karibu na wanao wa njia nyingi. Kufahamu wanayofanya na wakiwa na nani ili kuwaweka salama.

Msimu wa Krismasi unaponoga, ni ombi langu wazazi wawe macho. Kuna, mahayawani wengi ambao wako tayari kuchukua nafasi yoyote ipatikanayo, kuwadhuru wanao, licha ya umri wao.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti kunasa upya alama za waajiriwa wake

GWIJI WA WIKI: Catherine Kay

T L