• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
GWIJI WA WIKI: Catherine Kay

GWIJI WA WIKI: Catherine Kay

Na CHRIS ADUNGO

CATHERINE Kanini Muthini almaarufu Catherine Kay ni miongoni mwa waimbaji wa nyimbo za injili wanaotumia Kiswahili kueneza Ukristo na kuwasilisha dhamira mbalimbali zinazosawiri uhalisia wa maisha.

Upekee wake ulingoni ni ujuzi wa kuremba lugha kwa ufundi mkubwa na utajiri wa msamiati unaompa wepesi wa kuita maneno ya sifa kila anapojikuta katika majukwaa ya kumtukuza Mungu.

“Sawa na kazi nyinginezo za fasihi, uimbaji pia una uwezo wa kuibua uhalisia wa maisha ya jamii ambayo imemzaa, kumlea na kumkuza msanii,” anasema Catherine.

Ingawa umaarufu katika muziki ulianza kumwandama hivi majuzi, kipaji cha kuimba kilianza kujikuza ndani ya Catherine katika umri mdogo. Alikuwa tegemeo la makundi ya uimbaji kanisani na alishiriki mashindano ya ngazi na viwango tofauti shuleni.

Catherine alizaliwa katika eneo la Kambu, Kaunti ya Makueni. Alianza safari ya masomo katika shule ya msingi ya Kamulalani, Makueni, kabla ya kujiunga na shule ya msingi ya RC Mariakani iliyoko Kaunti ya Kwale (2000-2003).

Uchechefu wa karo ulimzimia ghafla mshumaa wa elimu akiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Mwavumbo, Kwale. Baada ya mama mzazi, Bi Esther Muthini, kuaga dunia mnamo Februari 2004, Catherine aliondoka Kwale na kurejea Makueni kuishi na nyanya yake, Bi Alice Kanini.

Alijifunza ususi na akaanza kusuka nywele vijijini kabla ya kuelekea Nairobi kufanya vibarua vya sampuli nyingi kuanzia 2005. Alihudumu baadaye katika kampuni mbili za kutengeneza na kupakia nywele bandia katika eneo la Industrial Area, Nairobi, hadi 2010.

Ilikuwa hadi 2020 alipojitosa kikamilifu katika fani ya muziki japo ndoto ya kuwa mwimbaji stadi ilianza kumtambalia utotoni.

‘Nilinde’ ni kibao cha kwanza alichokiachilia Agosti 2020. Wimbo huo, uliorekodiwa na Batoz Music Entertainment, ulimchochea kutoa ‘Salama Rohoni’, ‘Wastahili’‘Kwa Kalvari’‘Nonginya Neteele’‘Yahweh Anatenda’ na ‘Hujawahi Shindwa’‘Yes I Do’ na ‘You Reign’ ni nyimbo ambazo Catherine amezisana kwa Kiingereza.

Kubwa zaidi katika maazimio yake kisanaa ni kuhifadhi nyimbo zake katika albamu na kuendelea kuchomoa kibao kipya kila baada ya miezi mitatu. Anapania pia kupanua wigo wake wa ujasiriamali jijini Nairobi. Anauza vipodozi, mapambo na bidhaa mbalimbali za ulimbwende.

Matamanio yake mengine ni kushirikiana kikazi na baadhi ya wasanii ndani na nje ya Afrika Mashariki kutumia uimbaji kueneza Ukristo, kukuza maadili na kuipa jamii mwelekeo. Analenga pia kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanamuziki chipukizi kupitia utunzi wa nyimbo zinazokubalika kimataifa.

Catherine kwa sasa anashirikiana na makundi mbalimbali ya kijamii kuendesha kampeni maalumu za kusaidia mayatima na kusambaza viti vya magurudumu vya walemavu.

Anaistahi sana familia yake inayozidi kuiwekea kazi yake mshabaha na thamani. Kwa pamoja na mumewe, Bw Kennedy Kangangi, wamejaliwa watoto watatu – Shanice, Cyrus na Hadassah.

“Kipende unachokifanya na umtangulize Mungu katika kila hatua. Jitume, kuwa mkakamavu, mwenye nidhamu na mwingi wa subira,” anashauri.

You can share this post!

JURGEN NAMBEKA: Watoto walindwe na haki zao kuzingatiwa...

Jinsi nta inavyotumika kuitunza ngozi

T L