• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tudhibiti ndimi zetu kipindi hiki cha siasa za uchaguzi

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tudhibiti ndimi zetu kipindi hiki cha siasa za uchaguzi

Na ALI HASSAN

BAADA ya kumhimidi, kumshukuru na kumpwekesha Muumba wetu Mtukufu: Allah (SWT), Ijumaa ya leo naomba tuangazie joto na mihemko ya kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu.

Kila pembe, kila kona, ni kura na kula. Ala-kulihali kila mwanasiasa na wafuasi wake wanapania kujizolea kura zao.

Kipindi kama hiki ni kuwa wagombeaji wa nyadhifa mbali mbali za siasa wanatumia kila mbinu kuwatongoza wafuasi wao na pia kuwafurahisha wenye vyama na viongozi wao.

Miongoni mwa mbinu ambazo zinatumiwa na wanasiasa hawa na mawakala wao ni kutumia pesa, kabila, propaganda, chuki, chumvi na kila aina ya silaha. Hata ikibidi baadhi wanatumia maguvu, magumi, mateke na fujo za kila aina.

Wao wameamua afua ni mbili. Ashinde au ashinde. Kwa kila hali. Ndio maana baadhi utasikia wanatumia hata nguvu za kichawi, kishirikina na chochote kile, almradi achaguliwe mtu. Ya Rabi Mola wetu atunusuru. Hali si hali. Hali ni hamkani. Hatujiulizi kama kweli hayo yanayosemwa na wanasiasa yanaweza kutekelezeka? Hatujiulizi hawa wanasiasa wanaonadi sera zao za ukweli na urongo walikuwa wepi kabla, na kama kweli waliwahi kutimiza ahadi zao za kabla?

Wakati huu wa kampeni hata ndugu wanatusiana na kuchafuliana majina. Ndugu wa toka nitoke. Wanatusiana hadharani. Au hata mwana na baba wapo mirengo tofauti. Wanatofautiana kisiasa, kivyama na wanaishia kutukanana. Mbele za watu! Ulimi jamani! Kama hilo halitoshi, sasa hivi waja hawakumbuki dini. Almradi maslahi.

Hata viongozi wetu wa dini wameweka maslahi mbele. Mradi tumbo. Akija mtu na sera za dini, kujenga msikiti, kukarabati madrassa, kumlipa imamu au shekhe ama ustadh, hapawi kura. Anayeskilizwa ni mwenye hela. Subhannallah!

Mada hii tumeizungumzia katika ukumbi huu mara si moja. Na hatufai kukoma. Tukemee matamshi ya chuki kwa kila njia. Tusikubali ndimi kutuchonganisha. Waswahili wanasema heri ujikwae kidole wala sio ulimi. Athari na madhara yake ni makubwa mno! Neno halimezeki.

Au hatukumbuki mchafuko tuliyokuwa nayo baada ya uchaguzi wa mwaka 2007? Hadi nukta hii kesi zingali kuendelea huko The Hague. Dakika hii, tayari zipo kesi takriba 50 na za uchochezi. Baadhi ya kauli zikiwa ni za ‘madoadoa’, ‘kashfa za mauaji’ ‘wizi wa kura’na kauli nyinginezo chungu nzima.

Inakisiwa kuwa kaunti 23 zinakabiliwa na tishio la vurugu za uchaguzi! Ya Rabi tuwezeshe kuzidhibiti ndimi zetu.

Ijumaa Mubarak!

[email protected]

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Ubashiri hautokani na anachokijua msomaji

Vyuo vikuu vyashirikiana na UNESCO katika mpango wa O3 Plus

T L