• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
TAHARIRI: Serikali isiwe na huruma kwa wezi wa mitihani nchini

TAHARIRI: Serikali isiwe na huruma kwa wezi wa mitihani nchini

NA MHARIRI

SIKU ya Jumatatu jumla ya watahiniwa 831,015 wa kidato cha nne walianza mtihani wa kitaifa wa KCSE kote nchini.

Serikali imeahidi kudumisha ulinzi mkali kote nchini kuhakikisha kwamba mtihani huu unafanywa katika mazingira ya amani.

Hata hivyo, visa vya majaribio ya udanganyifu viliripotiwa katika baadhi ya maeneo.

Inasikitisha kwamba licha ya tahadhari ya serikali kuhusu athari za wizi wa mitihani pamoja na adhabu ambazo huandama vitendo hivi bado kuna watu ambao wemezinza vichwa wasisikie la mwadhini wala mteka maji msikitini.

Yamkini mifano mibaya kutoka kwa viongozi wetu imepenyeza katika jamii na kukita mizizi kiasi cha watu kushiriki udanganyifu bila woga wala soni.Inahuzunisha zaidi pale ambapo visa hivi vinaongozwa na walimu na wasimamizi wa mitihani.

Katika Kaunti ya Isiolo, mwalimu mkuu, msimamizi mkuu na wasimamizi wengine walikamatwa kwa jaribio la kushiriki katika udanganyifu wa mtihani unaoendelea wa KCSE.

Kamishna wa kaunti hiyo aliongeza kwamba vilevile simu nne zilizokuwa na mitihani zilipatikana zimefichwa katika choo katika shule ya upili ya Kinna.

Katika kaunti ya Busia George Barasa alipatikana akimfanyia babake mtihani wa kitaifa.

Barasa alibainika kuwa mwanafunzi wa zamani katika shule hiyo ya Bujwang’a.

Msusuru wa visa hivi unatia doa juhudi za maafisa, walimu na wanafunzi waadilifu ambao hulenga kuvuna kutokana na jasho lao halali.

Si ajabu kwamba mienendo hii ya wizi wa mitihani huendelezwa hadi ngazi za juu za elimu kama vile vyuo anuwai na vyuo vikuu.

Letu limekuwa taifa la wizi wa kila kitu. Si pesa za umma, si mitihani, si dawa hospitalini, si vipuri almuradi uozo huu umekita mizizi katika jamii.

Wizi wa mitihani ni tishio kwa maadili ya jamii na hivyo ustawi wa taifa zima.

Hii ni kwa sababu waajiri katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakilalamikia kupokea wahitimu ambao hawawezi kumudu changamoto zinazoambatana na taaluma ambazo wanadai kusomea.

Letu limekuwa taifa la kuwaandaa wafanyakazi chapwa, wale ambao hawajaiva wakatokota. Na kwa kweli hili halifai kushangaza kwa sababu haya ndiyo matokeo ya kuwa na wahitimu wanaotokana na udanganyifu wa mitihani katika asasi za elimu.

Ili kuepuka uozo huu kuendelea kukita mizizi katika jamii, serikali inafaa kuwachukulia wahusika hatua kali za kinidhamu ili wawe mfano kwa watu wengine.

Vilevile, tunatoa wito kwa serikali kuhakikisha maafisa wake wanakuwa mfano wa kuigwa katika jamii ili tulee kizazi ambacho kitaelekezwa kwa ustaarabu unaostahili.

You can share this post!

Usanii na kusanifisha machapisho umempa mapato kwa miaka 25...

Laini za simu ambazo bado hazijasajiliwa kuzimwa Aprili

T L