• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 9:50 AM
TAHARIRI: Serikali sharti itatue hili suala la mafuta kikamilifu

TAHARIRI: Serikali sharti itatue hili suala la mafuta kikamilifu

NA MHARIRI

KWA mara nyingine, taifa linakodolea macho mgogoro mpya kuhusu uhaba wa mafuta nchini.

Wiki mbili baada ya serikali, kupitia Waziri wa Kawi na Petroli Monica Juma kuita kikao na wanahabari na kutangaza kwamba usambazaji wa mafuta umerejeshwa katika hali ya kawaida kote nchini, sehemu mbali mbali zimeanza kushuhudia uhaba wa mafuta.

Wakazi katika maeneo ya Magharibi wanalia kukosa bidhaa hiyo muhimu huku maswali yakiibuka kwa nini hali kama hii inajirudia tena.

Miongoni mwa maelezo yaliyotolewa kuelezea kinachoendelea kwa sasa ni kwamba kampuni kubwa kubwa zinazoagiza mafuta kutoka nje zimeamua kuuza mafuta hayo katika vituo vyao pekee na wala sio kuuzia vituo vidogo vidogo vya mijini na mitaani.

Aidha, kuna habari kwamba wenye vituo vidogo wanaogopa kununua mafuta kutoka kwa kampuni hizo kubwa wakidai kuuziwa kwa bei ghali ambayo itawasababaishia hasara.

Sasa, habari kutoka kwa serikali jana ni kwamba itanunua mafuta kwa mkopo kutoka Dubai kwa kutumia shirika la kiserikali la National Oil halafu kulipa deni baadaye.

Inapanga kununua mafuta kwa kiwango cha asilimia 30 inayosambazwa nchini ili kuuzia wenye vituo vidogo vya mafuta kwa bei nafuu na kurudisha usambazaji mafuta katika hali shwari.

Ama kwa kweli, na licha ya kukejeliwa kwamba serikali ‘inafuliza’ hadi mafuta, mgala muue na haki mpe – angalau inaonekana kuchukua hatua licha ya kuwa hatua zenyewe zinazua hofu kuhusu uthabiti wa hali ya kifedha ndani ya serikali.

Kile ambacho serikali haitataka kikite mizizi ni huku kuonekana kwamba haina udhibiti wowote katika nguzo na nyanja muhimu katika taifa kama hii ya mafuta.

Mlipa ushuru amefanya kazi yake ya kulipa ushuru akitarajia huduma kupatikana. Serikali haitakuwa na mamlaka yoyote ya kutawala endapo haitaafiki jukumu lake ya kutoa huduma na uongozi haswa wakati ambapo mataifa mengine yanajitoa mhanga kukabiliana na athari za migogoro baina ya mataifa.

Itakumbukwa kwamba kufuatia uhaba wa mafuta kutokana na vikwazo vilivyowekewa Urusi kwa kuvamia Ukraine, mataifa kama vile Amerika yamechukua hatua kukinga raia wake kwa kuagiza kutumiwa kwa hifadhi yao ya mafuta badala ya kuagiza kutoka Urusi.

Kweli, Kenya hatuna viwango kama hivyo, lakini lazima itafute jinsi ikavyorudisha uhusiano mwema baina yake na waagizaji mafuta ambao utahusisha wao kulipwa mgao wao mapema inavyostahili.

You can share this post!

Jinsi Kibaki alivyoaibishwa hadharani baada ya kukosana na...

VITUKO: Chicharito hatarini kutemwa kufuatia ukware wake na...

T L