• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Tunateseka kwa kukosa mipangilio

TAHARIRI: Tunateseka kwa kukosa mipangilio

NA MHARIRI

HAKIKA taifa la Kenya tunapitia kipindi kigumu, na hii ni dhahiri kwa yeyote aliye mkazi wa nchi hii.

Ni kweli kuna changamoto duniani kote, mpaka Amerika na Ulaya wanalia hali ngumu ya maisha, lakini hali ya humu nchini bado ina upekee wa aina yake.

Majuzi kumechipuka video mitandaoni ya wahudumu wa kituo cha mafuta wakiimba na kushangilia kuona trela limeleta mafuta. Naam, sio wanunuzi wakiimba bali wahudumu wenyewe wanasherehekea tukio hilo kwa sababu ya tishio la kukosa kazi kutokana na kukauka kwa pampu za mafuta. Hapo ndipo tulipofikia kama taifa.

Upungufu umeshamiri katika idara nyingi. Si kwa mafuta, kwa maziwa hadi kwa mbolea. Wakulima wametangaziwa wakachukue mbolea ya bei nafuu iliyoletwa na serikali, lakini bado kuna vikwazo kuhusu kiasi ambacho mkulima anaruhusiwa kununua. Walianza na mifuko mitatu ya kilo 50 kwa mkulima, lakini malalamishi yakafanya waongeze hadi mifuko 10 ambayo bado haitoshi wakulima wakubwa.

Maziwa sasa hivi ukiingia maduka mengi, unakuta tangazo likisema usichukue zaidi ya pakiti tatu. Habari katika gazeti hili zinasema kampuni za maziwa zinakadiria hasara ya mamilioni ya pesa kufuatia kupungua kwa maziwa kwa hadi asilimia 50. Hii ina maana kuwa kitakachofuata ni mamia kuanza kufutwa kazi na familia kuhangaika.

Kwa upande wa mafuta ya petroli na dizeli, kampuni ya mabomba ya mafuta KPC imesema ina zaidi ya lita milioni mia mbili kwenye hifadhi yao, jambo linaloibua mjadala kuhusu jinsi nchi imejipata ikikumbwa na uhaba wa mafuta licha ya hifadhi hii kubwa.

Lakini unapoangalia kwa karibu visa hivi vyote, unagundua kwamba chanzo ni ama ukosefu wa mipango au mipangilio iliyotekelezwa kwa njia duni. Katika suala la mbolea, dalili zilianza kujitokeza mapema hata kabla ya vita Ukraine (vinavyodaiwa kusababisha uhaba). Tangu 2020, wakulima walikuwa wanalia bei ya juu ya mbolea. Kilichohitajika wakati huo ni kuwekwa mikakati wa kutatua sababu zilizokuwa zinachangia kupanda kwa bei. Lakini tulichoshuhudia ni kanuni ambazo ziliongeza ushuru wa bidhaa za ukulima na hivyo kuchangia kupandisha bei hata zaidi wakati bidhaa yenyewe ilipoanza kuadimika nchini.

Katika suala la maziwa, ukame umekuwa ukiripotiwa kwa miaka kadhaa iliyopita, lakini hakujakuwa na mikakati yoyote iliyofanikishwa kutafuta njia mbadala za kuendeleza uzalishaji. Na hili suala la mafuta, serikali ilifahamu fika kwamba inafaa kulipa ruzuku wauzaji mafuta lakini ikachelewa kwa zaidi ya mezi mitatu na kufanya wauzaji mafuta wakatae kununua mafuta ili kuja kuyasambazia umma.

You can share this post!

Mabilioni kukopwa kugharimia miradi

Yaya akana kuibia Benki Sh2.9Milioni

T L