• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Wasichana waokolewe dhidi ya mimba za mapema

TAHARIRI: Wasichana waokolewe dhidi ya mimba za mapema

NA MHARIRI

YEYOTE anayewapa watoto dawa za kupanga uzazi anajihatarisha kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.

Wale wanaojihusisha na biashara hii haramu watapata taabu sana wakikamatwa.

Lakini ingawa sheria hii ilitungwa kuwalinda wasichana wadogo, utoaji wa dawa za kupanga uzazi unaendelea bila kusitishwa na matokeo yake ni mabaya.

Kutoka kwa data ya hivi karibuni, ni dhahiri kwamba sheria haizingatiwi. Kulingana na takwimu zilizopo, msichana mmoja kati ya wanne wenye umri wa kati ya miaka 10 na 19 nchini Kenya ana mimba au amejifungua mtoto wake wa kwanza.

Masuala ya ujinsia wa vijana na afya ya uzazi mara nyingi yamezua mabishano kati ya wazazi, mamlaka, na viongozi wa kidini.

Kuwapatia dawa za uzazi ili kuzuia mimba ni ukiukaji wa Sheria ya Mtoto, ambayo inasisitiza haki na ulinzi wa vijana.

Kama Dkt Stephen Kaliti, mkuu wa afya ya uzazi katika makao makuu ya Wizara ya Afya ameelezea kwa uwazi kabisa kwamba kuwapa watoto dawa za uzazi ni kama kuwapa leseni ya ‘kuendesha miili yao wanavyotaka bila kuzingatia madhara’.

Tunakubaliana naye kwamba watoto wanapaswa kuruhusiwa kuwa watoto na sio watu wazima ambao wanaweza kuridhia uhusiano wa kimapenzi.

Hata hivyo, wazazi wengi hawawezi kuzungumzia suala hilo la mwiko na watoto wao—hasa baba na binti zao na mama na wana wao.

Katika mpangilio wa kitamaduni, shangazi na nyanya walitoa elimu juu ya ngono na uhusiano kwa wasichana wadogo jambo haliwezekani leo.

Changamoto ni kuja na mkakati unaoshughulikia unyeti wote kuhusu mada hii huku ukitoa matokeo yanayotarajiwa.

Njia nyingine, lakini ambayo makasisi na watu wengine wenye nia moja na mashirika wanaipinga, ni kutoa elimu ya ngono shuleni.

Hili halitabadilika hivi karibuni. Kwa hiyo, mamlaka lazima ishughulikie suala hilo kwa usikivu zaidi. Ni muhimu kwamba watoto wasiwe na mzigo wa mapema wa kuwa mama, ambalo ni jukumu zaidi ya uwezo wao wa kiakili na wa mwili.

Ni aibu kuwa machifu na manaibu wao ambao husuluhisha kesi za mimba za mapema kwa kukubali waathiriwa wapewe zawadi, kuolewa au kufidiwa wanaendeleza maovu hayo bila kupepesa macho.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, awachukulie hatua kwa sababu jambo hilo linahujumu mpango wa serikali wa kumaliza mimba za mapema nchini.

Akiongea kwenye mkutano na wakuu wa serikali wakiwemo makamishna wa kaunti 47 mjini Mombasa, alisema machifu watapewa mafunzo maalumu kuhusu uzuiaji wa visa vya dhuluma dhidi ya watoto.

Kulingana na takwimu za serikali, takriban wasichana 400,000 wa kati ya umri 10-19 walipachikwa mimba nchini huku asilimia 14 kati yao wakiozeshwa mwaka uliopita.

You can share this post!

Safari ya mwisho ya Kibaki yaanza rasmi

Wakenya waenzi rais aliyeweka maslahi ya taifa mbele ya yake

T L