• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
TAHARIRI: Wawaniaji urais watumie vyema fursa hii ambayo IEBC imewapatia

TAHARIRI: Wawaniaji urais watumie vyema fursa hii ambayo IEBC imewapatia

NA MHARIRI

HATUA iliyochukuliwa jana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwaongezea muda wawaniaji urais haifai kutumiwa vibaya.

Tume hiyo kupitia mwenyekiti wake, Wafula Chebukati, iliwapa wawaniaji hao pamoja na magavana, hadi Mei 16, wawasilishe majina ya wagombea wenza.

Awali, IEBC ilikuwa imepanga kwamba siku ya mwisho ya kufanya hivyo ingekua kesho Ijumaa, Aprili 28.

Wiki iliyopita, muungano wa Azimio uliiandikia barua IEBC, ukiitaka kuandaa kikao maalum ili kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu utaratibu iliyofuata katika kutoa tarehe hiyo.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alishikilia kuwa kulingana na uelewa wao wa sheria, wawaniaji urais wana hadi Mei 2 kuwateua wagombea-wenza wao.Upande wa mwaniaji wa Kenya Kwanza, Naibu Rais Dkt William Ruto pia ulikuwa na pingamizi kuhusu tarehe hiyo.

Kwa hivyo, mkutano wa jana Jumanne umewapa matumaini makubwa Dkt Ruto na kinara wa Muungano wa Azimio, Bw Raila Odinga.

Bw Chekubati alifafanua kuwa IEBC ilibadilisha tarehe hiyo baada ya kufanya mazungumzo na wawakilishi wa muungano wa Azimio-One Kenya na Kenya Kwanza.

Mabadiliko hayo yanalenga kuwapa vinara hao muda wa kujitayarisha katika kuwateua wawaniaji wenza.

Hata kama ni kweli kwamba kifungu cha 148 cha Katiba kinawapa wawaniaji urais uhuru wa kuteua wawaniaji wao, ni lazima shughuli hiyo ifuate muda uliowekwa na tume.

Suala la kuteua mgombea mwenza katu halifai kuwa siri. Kinachodhihirika katika uaombaji muda hapa, ni uoga kati ya wawaniaji wa mirengo mikuu, kuhusu chaguo la mwenzake.

Kwa muda sasa kumekuwa na pendekezo kuwa Bw Odinga amteue aliyekuwa mbunge wa Gichugu, Bi Martha Karua.

Upande wa Kenya Kwanza, kauli imekuwa sawa na hiyo. Kwamba Dkt Ruto amteue Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kuwania pamoja naye.

Kama watakubaliana na mapendekezo hayo au la, ni jambo tofauti.

Kile ambacho Wakenya wanasubiri kwa sasa ni kujua atakayekuwa mgombea mwenza.

Bila shaka Bw Odinga anaogopa kumkosea Bw Kalonzo Musyoka, ambaye Jumanne wafuasi wake Kaunti ya Tharaka Nithi walishinikiza kuwa kinara huyo wa Wiper apewe nafasi mara ya tatu.

Kwa upande wake, Dkt Ruto anaogopa kuwavunja moyo Bw Wycliffe Musalia Mudavadi (ANC) na wanasiasa Rigathi Gachagua na Mwangi Kinjuri kati yaw engine wanaomezea mate wadhifa huo.

Wanapaswa kuamua haraka, ili chelewa chelea yao isiathiri mipango ya maandalizi ya IEBC.

You can share this post!

Villarreal kuvizia Liverpool

Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza sasa kuripoti shuleni Mei 4...

T L