• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
WANTO WARUI: Serikali isaidie kutafuta suluhu kwa visa vya moto shuleni

WANTO WARUI: Serikali isaidie kutafuta suluhu kwa visa vya moto shuleni

NA WANTO WARUI

WASIWASI umezuka kwa wazazi na walimu wa shule za sekondari kutokana na visa vingi vya moto shuleni ambavyo vinaendelea kuripotiwa.

Juma lililopita mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari ya Thome, Kaunti ya Laikipia, alifariki kutokana na moto ulioteketeza bweni la shule.

Visa vingine kama hivyo viliripotiwa katika shule za sekondari za Muramati, St. Augustine Sirma na Shule ya Wasichana ya Loise.

Katika Kaunti ya Busia, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya John Osogo katika eneobunge la Budalangi walipoteza kila kitu baada ya moto kuzuka ndani ya bweni la ambalo huchukua wanafunzi 50.

Moto huo wa asubuhi haukuweza kuzimika upesi licha ya juhudi za wanafunzi na walimu. Kilichosababisha moto huo hakikujulikana mara moja. Huu ni moto wa pili kutokea katika shule hiyo mwaka huu.

Mapema mwaka huu, ofisi ya naibu wa mwalimu mkuu iliteketea na moto huo ukaharibu bidhaa za maelfu ya pesa. Kiini cha moto huo hakijabainika mpaka leo.

Katika kaunti hiyo hiyo, wanafunzi 60 wa shule ya wasichana ya Butula waliachwa bila chochote baada ya bweni lao kuteketea.

Moto huo ambao kiini chake hakikujulikana mara moja, uliwaacha wanafunzi na walimu vinywa wazi. Wazima moto kutoka eneo hilo walipofika walikuta moto umeshaharibu vitu vingi.

Muhula uliopita, Shule ya Sekondari ya Sigalame katika kaunti ndogo ya Samia, ilirekodi visa vinne vya moto, idadi ambayo ni kubwa mno kutokea katika shule moja.

Shule nyingine zilizoathirika ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Chamasiri katika kaunti ndogo ya Teso Kaskazini, Shule ya Nyamboboto na ile ya Ganjala zote kutoka kaunti hiyo ndogo ya Samia.

Pana hatari kubwa ikiwa Wizara ya Elimu haitaingilia suala hili na kuweza kubaini chanzo cha visa hivi vya moto.

Zaidi ya hapo, visa hivi vikomeshwe kabisa kwani vikiachiliwa jinsi vinavyoendelea tabia hii potovu inaweza kuenea katika shule nyingine na kuathiri masomo. Wakuu wa elimu katika kaunti husika wanafaa kufuatilia kesi hizi kwa kina kutoka shuleni kisha watafute suluhisho la kudumu.

Ikiwa ni walimu wakuu ambao wamezembea kazini, basi warekebishwe mara moja. Wakati mwingi hasa miaka ya awali baadhi ya migomo shuleni ilitekelezwa kuteketeza shule.

Katika kufanikisha na kuzima visa hivi, sheria pia ichukue mkondo wake ipasavyo na kuwaadhibu bila huruma wanaohusika.

Inapofika kwamba kuna visa vya aina hii, washikadau wote ni sharti waungane na kuingilia kati mapema ili kuziba ufa la sivyo watajenga ukuta.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Mataifa yazingatie uhuru wa kila mtu...

Kesi ya kukwepa ushuru wa mfinyo dhidi ya bwanyenye...

T L