• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
WANTO WARUI: Wanafunzi wafunzwe kuwa demokrasia ina mipaka

WANTO WARUI: Wanafunzi wafunzwe kuwa demokrasia ina mipaka

Na WANTO WARUI

JUMA lililopita tulishuhudia makabiliano baina ya wanafunzi na uongozi wa shule ambapo wanafunzi walitaka kutimiziwa matakwa yao kwa lazima.

Mabweni mengi ya shule za sekondari yaliteketezwa kwa kile kilichoonekana kama shinikizo la wanafunzi kwa serikali ili kuwaruhusu waende nyumbani. Hatimaye Wizara ya Elimu ilisalimu amri kwa kutangaza kuwe na likizo fupi ya katikati ya muhula kuanzia Ijumaa tarehe 19-11-2021 hadi Jumanne tarehe 23-11-2021, kinyume na ilivyokuwa imepanga awali.

Ingawa wazo la kuwapa likizo fupi ya kati ya muhula ni zuri na lilikuwa limepuuzwa kwa maksudi, wanafunzi kulazimisha serikali kufanya watakavyo kwa vitendo vya utovu wa nidhamu hasa kuchoma mabweni, si jambo jema hata kidogo na halistahili kufumbiwa macho.

Hawa ni wanafunzi ambao hawana uwezo wa kujiamulia mambo kwa uhakika na wako chini ya utawala na uangalizi wa serikali. Kulazimisha serikali iratibu kalenda ya masomo watakavyo wao ni makosa.

Ikiwa wanafunzi hawa wanazua fujo na vurugu wakiwa watoto, je, itakuwaje wakiwa wakubwa? Tayari wanadhani kuwa njia bora zaidi ya kutaka kutimiziwa mahitaji yao ni kutumia fujo, na hivyo ndivyo watakavyokuwa wakikua kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

Kwao sasa wanajua wameshinda na wamejua lugha ya kutaka kutimiziwa haja ni kuzua fujo na kuharibu mali – aibu gani?Serikali inafaa kusimama kidete na kutumia uwezo wake kutoa maamuzi yafaayo bali si kushinikizwa na wanafunzi kupangua mipango yake.

Sheria zinafaa kuwekwa na kuzingatiwa kikamilifu. Wanafunzi wanafaa kuambiwa na kufunzwa kuwa kudai haki zao kwa kukiuka haki za wengine na kuharibu mali ni hatia inayotolewa adhabu za kisheria. Wanafunzi wanaotekeleza uovu huu wafikishwe mahakamani na wahukumiwe kulingana na sheria.

Hawa watakuwa funzo kwa wengine wanaofikiria kutenda uhuni kama huo shuleni.Aidha serikali inafaa kupiga darubini upya mbinu zinazotumiwa kudumisha nidhamu shuleni. Ikiwa kwa mfano, ushauri nasaha hauzai matunda, basi walimu wahimizwe zaidi kuwashauri wanafunzi au Somo la Ushauri nasaha litiwe katika silabasi.

Kando na hayo, kuwe na njia mbadala za kuwarekebisha wanafunzi. Kwa mfano, mojawapo ya njia nzuri ya kurekebisha tabia za watu ni kuwashirikisha katika kuunda sheria zinazowatawala wao wenyewe na kuweka adhabu zitakazotolewa iwapo mtu atakiuka sheria hizo.

Katika kufanya hivi shuleni, wanafunzi watahisi kuwa sheria ni zao na utawala ni wao, hivyo basi hawatapenda kukiuka yale waliojitungia wao wenyewe. Hili linaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa tabia za utovu wa nidhamu shuleni.

Kila kiumbe kilichowekewa sheria na kiumbe kingine huhisi kuwa kinanyanyaswa. Hatimaye, ni vyema wanafunzi waelewe kuwa hakuna demokrasia isiyo mipaka yake ambayo haifai kukiukwa kamwe!

You can share this post!

Kaunti ya Nairobi yaanzisha mfumo mpya wa kulipia huduma

CHARLES WASONGA: KEMSA yadai wafanyakazi wa chini wasifutwe...

T L