• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Aguero kuyoyomea Barcelona mwishoni mwa msimu

Aguero kuyoyomea Barcelona mwishoni mwa msimu

Na MASHIRIKA

FOWADI Sergio Aguero ameafikiana na Barcelona ambao sasa watamsajili kwa mkataba wa miaka miwili mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Aguero, 32, atabanduka ugani Etihad bila ada yoyote baada ya kandarasi yake ya sasa na Man-City kutamatika rasmi mwishoni mwa muhula huu. Nyota huyo raia wa Argentina amefungia Man-City jumla ya mabao 258 kutokana na mechi 388.

Ingawa Barcelona wamefichua mpango wa kupunguza gharama ya matumizi, wameshawishika kujitwalia huduma za Aguero kwa matarajio kwamba atashirikiana vilivyo na Lionel Messi na Antoine Griezmann katika safu yao ya mbele.

Aguero ambaye kwa sasa anashikilia nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), ni rafiki wa karibu wa Messi ambaye amekuwa akishirikiana naye katika timu ya taifa ya Argentina.

Barcelona wamesajili matokeo mseto katika kampeni za msimu huu chini ya kocha raia wa Uholanzi, Ronald Koeman. Walibanduliwa na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), wakatwaa taji la Copa del Rey na kwa sasa wanakamata nafasi ya tatu kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Pengo la alama nne linatamalaki kati yao na viongozi Atletico Madrid wanaoselelea kileleni kwa pointi 80.

Barcelona pia wamefichua orodha ya wanasoka sita ambao kocha Koeman amewapendekezea kusajili mwishoni mwa msimu huu.

Huku rais mpya wa kikosi hicho, Joan Laporta akiwa mwingi wa matumaini kwamba kigogo Messi atarefusha mkataba wake ugani Camp Nou, kinara huyo amekiri kwamba wanahitaji kujisuka upya kwa ajili ya misimu ijayo.

Kwa mujibu wa gazeti la Sport nchini Uhispania, fowadi Erling Braut Haaland ni miongoni mwa wanasoka wanaoviziwa na Barcelona ambao tayari wamekutana na baba wa nyota huyo raia wa Norway, Alf-Inge pamoja na wakala wake, Mino Raiola.

Haaland, 20, amefungia waajiri wake Borussia Dortmund jumla ya mabao 39 kutokana na mechi 39 za msimu huu na anahusishwa pakubwa na Man-City na Real Madrid.

Kulingana na gazeti la Mundo Deportivo, Barcelona wako pazuri zaidi kujinasia maarifa ya Haaland ambaye amekuwa na matamanio ya kucheza pamoja na Messi tangu utotoni.

Koeman, 58, anamezea pia maarifa ya fowadi wa zamani wa Manchester United, Memphis Depay, aliyewahi kuwa chini ya uelekezi wake katika timu ya taifa ya Uholanzi. Sawa na Aguero, mkatabwa wa sasa wa Depay na Olympique Lyon ya Ufaransa unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Depay, 27, amefungia Lyon jumla ya mabao 19 na kuchangia mengine 10 kutokana na mechi 35 zilizopita za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Sogora mwingine anayehemewa na Barcelona ni fowadi Lautaro Martinez ambaye kwa pamoja na Romelu Lukaku, amekuwa tegemeo kubwa kambini mwa Inter Milan ambao ni mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Haja ya kuendelea kushirikiana na Messi katika ngazi ya klabu sawa na jinsi ilivyo katika kiwango cha timu ya taifa huenda ikamchochea Martinez kuyoyomea Barcelona.

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 23 amefungia Inter jumla ya mabao 15 na kuchangia mengine manane kwenye kampeni za Serie A muhula huu.

Masogora wengine wanaohusishwa pakubwa na Barcelona ni kiungo matata wa Liverpool, Georginio Wijnaldum na beki Eric Garcia wa Man-City.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Koome atofautiana na Maraga

BBI: Majaji watano walivyozima midundo ya Reggae