• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
AK yaongeza Team Kenya ya mbio za nyika kutoka wanariadha 32 hadi 40

AK yaongeza Team Kenya ya mbio za nyika kutoka wanariadha 32 hadi 40

NA AYUMBA AYODI

SHIRIKISHO la Riadha Kenya (AK) limeongeza wanariadha wanane katika kikosi chake cha taifa kitakachoshiriki Mbio za Nyika za Dunia mjini Bathurst, Australia mnamo Februari 18 mwaka 2023.

Mkurugenzi wa AK wa mashindano Paul Mutwii amefichua Jumatano kuwa wanane hao watakuwa katika orodha ya watakaosubiri kujaza nafasi ya yeyote atakayeumia ama kujiondoa.

“Tumesalia na karibu miezi miwili kabla ya mashindano na huo ni muda mrefu sana,” alisema Mutwii, akiongeza kuwa wanane hao watajiunga na kambi ya mazoezi Januari 10 katika eneo litakalotangazwa baadaye.

Mwanajeshi wa KDF, Collins Koros, ambaye anarejea kutoka mkekani, na Hillary Kipchirchir kutoka Kaptagat, wamejumuishwa katika mbio za kilomita 10 za wanaume.

Bingwa wa KDF mbio za mita 10,000 mwaka 2021 Koros, 31, na Kipchirchir, walikamata nafasi ya saba na nane wakati wa mashindano ya kuchagua timu ya taifa katika Chuo cha Mafunzo ya Magereza mjini Ruiru, Kiambu.

Mwanajeshi wa KDF, Cynthia Chepng’eno, 22, aliyemaliza katika nafasi ya saba, ni mwanariadha wa pekee kuongezwa katika kitengo cha mbio za kilomita 10 cha kinadada.

Stephen Masinget na Daniel Kinyanjui waliokamata nafasi ya 10 na 13 mtawalia, wameingia timu ya wanaume wasiozidi umri wa miaka 20 itakayoshiriki mbio za kilomita nane.

Dada mdogo wa mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon Brigid Kosgei, Pamela Kosgei kutoka Elgeyo Marakwet na Diana Chepkemoi (Lemotit) wameongezwa katika mbio za wanawake wasiozidi umri wa miaka 20 itakayoshiriki mbio za kilomita sita.

Pamela na Chepkemoi walikuwa nambari saba na nane wakati wa kuchaguliwa kwa timu ya Kenya. Pamela alikuwa katika timu ya Kenya iliyoshiriki Riadha za Dunia za Under-20 mjini Cali, Colombia mwezi Agosti. Alitimka mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji na kumaliza katika nafasi ya tano.

Betty Chelangat, ambaye alikamilisha katika nafasi ya nne katika mbio za kilomita mbili, amejumuishwa katika timu ya mbio za mseto za kupokezana vijiti. Team Kenya sasa ina jumla ya wanariadha 40.

Mutwii alifichua kuwa kambi haitakuwa Kigari, Embu ama Nairobi, lakini kamati ya kiufundi inaweza kuchagua maeneo matatu kufanyia mazoezi kutoka orodha ya Nandi, Kericho na Machakos.

“Watazingatia tabianchi na barabara za mashindano. Tunachunguza vitu hivyo vyote ili tufikie uamuzi mzuri,” alisema Mutwii.

Kikosi cha Kenya:

Kikosi cha Kenya: Wanaume (10km) – Sebastian Kimaru, Daniel Simiu, Kibiwott Kandie, Emmanuel Kiprop, Nicholas Kipkorior, Geoffrey Kamworor. Watimkaji wa akiba ­- Collins Koros, Hillary Kipchirchir; Wanawake (10km) – Grace Loibach, Edinah Jebitiok, Irene Cheptai, Agnes Jebet, Viola Chepng’eno, Emily Chebet, Beatrice Chebet. Mkimbiaji wa akiba – Cynthia Chepng’eno; Wanaume (8km) – Ismael Kirui, Reynold Kipkorir, Dennis Kipkirui, Raphael Dabash, Gideon Kipng’etich, Charles Rotich. Watimkaji wa akiba – Stephen Masinget, Daniel Kinyanjui; Wanawake (6km) – Faith Cherotich, Sheila Chebet, Joyline Chepkemoi, Nancy Cheriop, Marion Chepng’etich, Diana Cherotich. Wakiambiaji wa ziada – Pamela Kosgei, Diana Chepkemoi; Wanaume (2km mbio mseto) – Emmanuel Wanyonyi, Daniel Munguti, Mathew Kipsang, Abel Kipsang; Wanawake (2km mbio seto) – Brenda Chebet, Miriam Cherop, Beatrice Chepkoech. Mtimkaji wa akiba – Betty Chelangat.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

STAK yataka kampuni zote za mbegu nchini zisajiliwe chini...

Kanisa lalaumu wazazi kwa kuongezeka kwa usagaji na ushoga

T L