• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Arsenal kumtia fowadi Alexandre Lacazette mnadani ndipo wapate fedha za kujisuka upya

Arsenal kumtia fowadi Alexandre Lacazette mnadani ndipo wapate fedha za kujisuka upya

Na MASHIRIKA

ARSENAL wamefichua mpango wa kumtia mshambuliaji Alexandre Lacazette mnadani ili wapate fedha za kuwawezesha kujisuka upya kwa ajili ya msimu ujao wa 2021-22.

Mkataba wa sasa kati ya Arsenal na Lacazette unatarajiwa kutamatika rasmi baada ya mwaka mmoja ujao na kocha Mikel Arteta amesema asingetaka sogora huyo aondoke uwanjani Emirates bila ada yoyote. Lacazette alisajiliwa na Arsenal kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa kwa Sh7.2 bilioni mnamo 2017.

Hivyo, Arsenal wako radhi kumuuza Lacazette hata kwa bei ya kutupa ili wajipunguzie gharama ya Sh28 milioni ambazo kwa sasa wanamlipa sogora huyo raia wa Ufaransa mwishoni mwa kila mwezi.

Fedha hizo zinamfanya Lacazette kuwa mwanasoka wa tatu anayedumishwa kwa mshahara wa juu zaidi kambini mwa Arsenal baada ya Pierre-Emerick Aubameyang na Thomas Partey ambao hutia mfukoni kima cha Sh39 milioni kwa wiki kila mmoja.

Kimshahara, mgongo wa Lacazatte unasomwa kwa karibu sana na beki Hector Bellerin, kipa Bernd Leno na kiungo Granit Xhaka.

“Arsenal wana kiu ya kuuza Lacazette ili wapunguze gharama ya matumizi na pia kupata fedha za kuwawezesha kusajili wanasoka mahiri watakaofanikisha malengo yao ya muhula ujao,” akasema Arteta.

Kati ya wanasoka hao wanaomezewa mate na Arsenal ni Ben White wa Brighton ambaye anatarajiwa kuwa kizibo cha David Luiz. White ambaye ni raia wa Uingereza atawagharimu Arsenal kima cha Sh7.8 bilioni. Kikosi hicho ambacho tayari kimemsajili beki Nuno Tavares kwa Sh1 bilioni, pia kinavizia difenda Sambi Lokonga wa klabu ya Anderlecht na timu ya taifa ya Ubelgiji.

Arteta amefichua kwamba waajiri wake wamemtengea pia kima cha Sh11 bilioni kwa ajili ya kumsajili kiungo mbunifu atakayekuwa akiwajibishwa nyuma ya wavamizi wakuu kambini mwa Arsenal.

Mbali na Lacazette, wanasoka wengine ambao wataagana na Arsenal muhula huu ni Granit Xhaka, Lucas Torreira na Matteo Guendouzi. Kuondoka kwao kutapisha chipukizi Eddie Nketiah na Folarin Balogun kudhihirisha utajiri wa vipaji vyao uwanjani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Bandari ya Lamu kuanza kutumiwa kuingiza mafuta ya nazi

Mwanariadha Mkenya ajiondoa Olimpiki kwa kukosa vipimo...