• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Mwanariadha Mkenya ajiondoa Olimpiki kwa kukosa vipimo halali vya dawa za kusisimua misuli

Mwanariadha Mkenya ajiondoa Olimpiki kwa kukosa vipimo halali vya dawa za kusisimua misuli

AYUMBA AYODI na GEOFFREY ANENE

KENYA haitawakilishwa katika mbio za mita 400 za kuruka viunzi kwenye Olimpiki hapo Julai 23 hadi Agosti 8 baada ya mtimkaji wa kitengo hicho Mpoke Moitalel kujiondoa Jumapili.

Mkazi huyo wa Amerika alitangaza kujiondoa kwake kupitia mitandao yake ya kijamii na kuomba Wakenya msamaha kwa kutotimiza baadhi ya mahitaji ya Shirikisho la Riadha Duniani (WA).

Huku Kenya ikiwa katika kategoria ya A ambayo ni ya mataifa yanayomulikwa zaidi na WA na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli duniani (WADA), wanariadha wote wa Kenya wanaoshiriki mashindano makubwa lazima wapimwe mara tatu nje ya mashindano matumizi ya pufya katika kipindi cha miezi 10 na pia majuma matatu kabla ya mashindano.

Mojawapo ya vipimo hivyo lazima viwe vya damu.

“Nawaomba msamaha kuwa siwezi kushiriki Olimpiki za Tokyo 2020, ingawa nimekuwa nikijitayarisha vyema licha ya changamoto zote nilizopitia kabla ya kufikia muda unaotakikana kuweza kushiriki,” alitanguliza Mpoke kwenye ukarasa wake wa Facebook hapo Julai 4.

Mpoke alisema kuwa alipimwa mara tatu inavyohitajika na kutuma matokeo yake kwa Shirikisho la Riadha Kenya (AK).

Mpoke alisema kuwa habari kuwa maafisa wa WADA walifika nyumbani wake mjini Texas kumpima si za kweli.

“Hakuna mtu alikuja kwangu kwa sababu nilikuwa nyumbani nikijiandaa kufanya mtihani wangu wa mwisho wa Chuo Kikuu na sikupokea simu yoyote,” alieleza Mpoke kabla ya kuongeza, “Nasikitika sana, lakini natumai kuwaona nyote msimu ujao.”

Meneja Mkuu wa timu ya Kenya ya Olimpiki za Tokyo, Barnaba Korir alisema kuwa haijawezekana Mpoke kutimiza masharti ya WADA.

Korir alisema kuwa, ingawa Mpokea aliwasilisha vipimo vya nje ya mashindano, waliompima hawakuwa wameidhinishwa na WADA wala Shirikisho la Riadha Duniani.

“Vipimo anavyozungumzia vilifanywa na Chuo Kikuu anakosomea ambacho hakiruhusiwi na Kitengo cha Maadili cha Riadha (AIU) na WADA,” alisema Korir.

Afisa huyo alieleza kuwa kushughulikia utata huo, AK iliwasiliana na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya la Kenya (ADAK) ambalo liliwasiliana na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya la Amerika (USADA) ili vipimo vingine vifanywe kwa muda unaofaa.

“Mpoke hakupatikana walipoenda kumpima,” alisema Korir ambaye alionyesha stakabadhi kutoka USADA zilizoonyesha kuwa walibisha mlango wake nyumba yake mara tano pamoja na kuita jina lake, lakini hakujibu.

Kenya iliwakilishwa kwenye mbio za mita 400 za kuruka viunzi na Boniface Mucheru na Vincent Koskei mwaka 2012 mjini London, Uingereza na Mucheru na ndugu Aron Koech na Nicholas Bett mjini Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016.

Mucheru alizoa medali ya fedha mjini Rio kwa rekodi ya kitaifa ya sekunde 47.78 nyuma ya Mwamerika Kerron Clement (47.73) na mbele ya Mturuki Yasmani Copello (49.52).

You can share this post!

Arsenal kumtia fowadi Alexandre Lacazette mnadani ndipo...

Kipa Jordan Pickford wa Uingereza afikia rekodi ya jagina...