• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Arsenal kuwatoa chipukizi Willock, Nketiah na Reiss-Nelson kwa mkopo mwezi huu wa Januari 2021

Arsenal kuwatoa chipukizi Willock, Nketiah na Reiss-Nelson kwa mkopo mwezi huu wa Januari 2021

Na MASHIRIKA

MAKINDA watatu wa Arsenal – Joe Willock, Reiss-Nelson na Eddie Nketiah watatumwa kwingineko kwa mkopo mwezi huu wa Januari ili wapate muda zaidi wa kujikuza kitaaluma kabla ya kurejea uwanjani Emirates.

Chipukizi hao wamekosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha sasa cha Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta ambaye analenga kupunguza zaidi idadi ya wanasoka wake ili kutoa fursa ya kusajiliwa kwa Isco na Houssem Aouar kutoka Real Madrid na Olympique Lyon mtawalia.

Nelsin, 21, aliwahi kutumwa kwa mkopo wa mwaka mmoja kambini mwa Hoffenheim ya Ujerumani mnamo 2018-19. Tangu arejee Emirates, amewajibishwa na Arsenal mara saba pekee msimu huu huku akitokea benchi mara mbili kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kwa upande wake, Willock, 21, amechezeshwa mara 13 ila kwa wingi zaidi katika mashindano ya League Cup na Europa League. Ni Nketiah, 21, ndiye amewajibishwa zaidi na waajiri wake hao baada ya kupangwa kikosini mara 20.

Hata hivyo, fowadi huyo aliyechezea Leeds United ka mkopo mnamo 2019-20, amepangwa katika kikosi cha kwanza kwenye EPL mara tatu pekee.

Kati ya chipukizi wengine ambao Arteta amefichua kwamba hawapo katika mipango yake kwa sasa ni beki chipukizi William Saliba, 19, ambaye kwa sasa anahemewa na Leicester City (Uingereza) na Nice (Ufaransa).

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, Saliba anahusishwa pia na vikosi kadhaa za Ligi Kuu nchini Ujerumani na Uholanzi japo Leicester ndio waliopo pazuri zaidi kumtwaa baada ya Brendan Rodgers kumsajili Wesley Fofana aliyewahi kucheza pamoja na Saliba kambini mwa Saint-Etienne nchini Ufaransa.

Baada ya kumtuma beki Sead Kolasinac kuchezea Schalke ya Ujerumani kwa mkopo, Arteta analenga kuwatema pia wachezaji Mesut Ozil, Shkodran Mustafi na Sokratis Papastathopoulos anayewaniwa na Fenerbahce ya Uturuki. Beki Konstantinos Mavropanos (Stuttgart, Ujerumani), kiungo Lucas Torreira (Atletico Madrid, Uhispania) na kiungo Matteo Guendouzi (Hertha Berlin, Ujerumani) ni miongoni mwa wanasoka waliotolewa na Arsenal kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21.

  • Tags

You can share this post!

SERIE A: Martinez afunga mabao matatu na kusaidia Inter...

De Bruyne kutia saini mkataba mpya Manchester City na...