• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Arsenal wadhalilisha Sevilla huku Man-United wakipigwa na Atletico Madrid kirafiki

Arsenal wadhalilisha Sevilla huku Man-United wakipigwa na Atletico Madrid kirafiki

 Na MASHIRIKA

GABRIEL Jesus alifunga mabao matatu katika mchuano wake wa kwanza ugani Emirates na kusaidia Arsenal kupepeta Sevilla 6-0 katika pambamo la Emirates Cup mnamo Jumamosi.

Bao lake la tatu lilikuja katika dakika ya 77.

Bukayo Saka alipachika wavuni magoli mawili huku The Gunners wakijiweka kifua mbele kwa mabao 4-0 dhidi ya Sevilla chini ya dakika 19. Bao jingine la Arsenal lilijazwa kimiani na mshambuliaji Eddie Nketiah.

Kwingineko, Manchester United walipokezwa kichapo cha 1-0 na Atletico Madrid katika uwanja wa Ullevaal jijini Oslo, Norway. Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Atletico lilifungwa na Joao Felix kabla ya kiungo Fred wa Man-United kuonyeshwa kadi nyekundu.

Nchini Israel, mpira wa kona uliopigwa na Paulo Dybala ulisaidia Roger Ibanez kufungia AS Roma bao la pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspur.

Kocha Antonio Conte wa Spurs alipanga kikosi cha wanasoka wa haiba dhidi ya Roma wanaonolewa na kocha Jose Mounrinho. Sajili wapya Ivan Perisic na Yves Bissouma waliunga kikosi cha kwanza cha Spurs kilichojivunia pia maarifa ya wavamizi Harry Kane na Son Heung-min

Beki Clement Lenglet, mshambuliaji Richarlison Andrade na kipa Fraser Forster ambao wote walijiunga na Spurs muhula huu, waliwajibishwa na Spurs katika kipindi cha pili.

Ushindi wa Arsenal dhidi ya Sevilla ulikamilisha kipindi cha maandalizi murua kwa ajili ya msimu mpya wa 2022-23 ambapo Jesus aliyetokea Manchester City kwa Sh6.4 bilioni, amefunga mabao saba.

Kwa upande wao, Chelsea walipepeta Udinese 2-0 baada ya kufungiwa mabao yao na Ruben Loftus-Cheek na Hakim Ziyech uwanjani Dacia Arena. Kikosi kingine tofauti cha Chelsea kilikuwa kimetandika Udinese 3-1 katika uwanja uo huo wa Dacia Arena mnamo Julai 29, 2022.

Brighton nao walicharaza Espanyol ya Uhispania 5-1 ugani Amex baada ya kufungiwa mabao yao na Adam Webster, Lewis Dunk na Leandro Trossard aliyecheka na nyavu mara tatu. Brighton hawakumwajibisha beki Marc Cucurella anayewaniwa na Manchester City katika mechi hiyo.

Wakati uo huo, Bournemouth walipokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Real Sociedad ya Uhispania iliyofunga mabao kupitia kwa Mikel Merino na Igor Zubeldia. Bournemouth walifutiwa machozi na Junior Stanislas.

Callum Wilson na Allan Saint-Maximin walifunga mabao katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Newcastle United dhidi ya Athletic Bilbao 2-1. Bryan Mbeumo naye alicheka na nyavu katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na waajiri wake Brentford dhidi ya Real Betis.

Crystal Palace walivuna ushindi wa 4-2 dhidi ya Montpellier, huku mabao ya kikosi hicho cha kocha Patrick Vieira yakifumwa wavuni na Wilfried Zaha, Marc Guehi na Odsonne Edouard aliyefunga mawili.

Ingawa sajili mpya wa Southampton, Joe Aribo alifunga bao, mchango wake ulishindwa kuzuia Villarreal ya Uhispania kuwatandika 2-1.

Nchini Ufaransa, beki mpya wa Aston Villa, Diego Carlos alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia kikosi hicho cha kocha Steven Gerrard kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Rennes 2-1.

West Ham walilazimishiwa sare tasa na Lens, huku Wolves wakitoshana nguvu na Sporting Lisbon ya Ureno kwa sare ya 1-1.

Nottingham Forest waliorejea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Valencia licha ya kujivunia huduma za sajili mpya, Jesse Lingard.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mtaalamu ahimiza wakulima wakumbatie mifumo ya kuvuna maji

Shule kufungwa kwa muda kuanzia kesho Jumanne hadi Agosti...

T L