• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 9:50 AM
Aubameyang afunga mabao matatu na kusaidia Arsenal kuponda West Brom kwenye Carabao Cup

Aubameyang afunga mabao matatu na kusaidia Arsenal kuponda West Brom kwenye Carabao Cup

Na MASHIRIKA

PIERRE-Emerick Aubameyang alifunga mabao matatu na kusaidia waajiri wake Arsenal kupepeta West Bromwich Albion 6-0 katika mechi ya Carabao Cup mnamo Jumatano usiku uwanjani The Hawthorns.

Ushindi huo ambao ulikuwa wa kwanza kwa Arsenal kuvuna msimu huu, uliwawezesha kuingia raundi ya tatu ya kipute cha Carabao Cup.

Katika mchuano huo ambao ulikuwa wa kwanza kwa Aubameyang kuchezea Arsenal msimu huu, ulishuhudia fowadi huyo raia wa Gabon akipachika wavuni magoli mawili katika kipindi cha kwanza.

Alifunga bao lake la tatu katika dakika ya 62 baada ya Nicolas Pepe kutikisa nyavu za wenyeji wao na kuwap Arsenal bao la tatu mwanzoni mwa kipindi cha pili. Mabao mengine ya Arsenal yalijazwa kimiani kupitia Bukayo Saka na Alexandre Lacazette aliyetokea benchi katika kipindi cha pili.

Arsenal wangalifunga mabao zaidi ila Pepe na Martin Odegaard wakapoteza nafasi kadhaa za wazi katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Chini ya kocha Valerian Ismael, West Brom walichezesha wanasoka sita kwa mara ya kwanza katika kikosi chao na watano kati yao walikuwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 19.

Mechi dhidi ya West Brom almaarufu ‘The Baggies’ iliwapa Arsenal fursa ya kumwajibisha kipa Aaron Ramsdale kwa mara ya kwanza tangu abanduke kambini mwa Sheffield United.

Ushindi huo wa Arsenal unatarajiwa kumpunguzia kocha Mikel Arteta presha tele kadri anavyokiandaa kikosi chake kumenyana na Manchester City kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Agosti 29, 2021 ugani Etihad. Arsenal watashuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo baada ya kupoteza mechi mbili za ufunguzi dhidi ya limbukeni Brentford (2-0) na Chelsea (2-0).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Zappacosta aondoka Chelsea na kurejea Italia kuchezea...

Real Madrid watoa ofa ya Sh21.3 bilioni kushawishi Kylian...