• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Beckham pabaya kikosi chake kukiuka kanuni za MLS kiliposajili kiungo Blaise Matuidi

Beckham pabaya kikosi chake kukiuka kanuni za MLS kiliposajili kiungo Blaise Matuidi

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha Inter Miami kinachomilikiwa na mwanasoka wa zamani wa Manchester United, David Beckham, kilikiuka kanuni za Major League Soccer (MLS) nchini Amerika kilipomsajili kiungo raia wa Ufaransa, Blaise Matuidi kutoka Juventus mnamo 2020.

Kwa mujibu wa MLS, Matuidi, 34, alisajiliwa kwa kiasi kikubwa cha pesa kuliko kile kilichostahili na hatua hiyo iliwapa Inter Miami mchezaji wa nne wa kigeni kuliko watatu wanaokubaliwa.

Japo kikosi chochote kinachoshiriki MLS kina uhuru wa kusajili mchezaji wa “ziada” (mbali na watatu wanaokubaliwa), sogora huyo hastahili kutiwa kwenye orodha ya wanaopokezwa mshahara, bonasi au marupurupu na MLS.

Sheria hiyo inayoitwa “Beckham rule” ilianzishwa katika MLS mnamo 2007 baada ya mwanasoka huyo wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Uingereza kusajiliwa na Los Angeles Galaxy.

Wakati huo, Beckham alipewa idhini ya kupanua umiliki wa kikosi cha Inter Miami na akawa miongoni mwa washikadau wakuu wa klabu hiyo iliyoanza kunogesha soka ya MLS mnamo Machi 2020.

Katika taarifa yake, MLS imesema kwamba Matuidi ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia, alikuwa ameorodheshwa kimakosa na waajiri wake kuwa sehemu ya wanasoka wanaostahili kulipwa mshahara kutokana na mgao wa fedha zinazotolewa kwa washiriki wa soka ya MLS.

Aidha, kiasi cha fedha anazolipwa ni za kiwango cha juu na alistahili kutiwa kwenye orodha ya wanasoka wa “ziada” kambini mwa Inter Miami FC ambao kwa sasa wanakodolea adhabu kali kutoka MLS.

Ilivyo kwa sasa, Matuidi anastahili kujumuishwa kwa pamoja na mshambuliaji wa Argentina Gonzalo Higuain na kiungo wa Mexico, Rodolfo Pizarro, kwenye orodha ya wachezaji wa “ziada” kambini mwa Inter Miami.

Ili kumdumisha Matuidi kambini mwao, Inter Miami watalazimika kuweka mezani kiasi kikubwa cha fedha ili kufanikisha uhamisho wa kiungo raia wa Argentina, Matias Pellegrini hadi kambini mwa Fort Lauderdale kwa mkopo.

Inter Miami kwa sasa wanatiwa makali na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Uingereza, Phil Nevile aliyewahi kucheza pamoja na Beckham kambini mwa Man-United.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

AKILIMALI: Jinsi ufinyanzi inavyomfaidi

Kocha Ronald Koeman kufutwa kazi asiposhindia Barcelona...