• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kocha Ronald Koeman kufutwa kazi asiposhindia Barcelona taji lolote msimu huu

Kocha Ronald Koeman kufutwa kazi asiposhindia Barcelona taji lolote msimu huu

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Ronald Koeman wa Barcelona amefutilia mbali tetesi atafutwa kazi uwanjani Camp Nou iwapo kikosi chake kitashindwa na Athletic Bilbao kwenye fainali ya Copa del Rey msimu huu.

Koeman, 58, aliajiriwa na Barcelona kwa mkataba wa miaka miwili mwanzoni mwa msimu wa 2020-21 na ameongoza kikosi chake kusajili matokeo mseto kwenye mapambano mbalimbali ya hadi kufikia sasa msimu huu.

Licha ya ufufuo ambao umeshuhudia Barcelona wakifukuzana na Atletico Madrid na Real Madrid kwenye vita vya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), kikosi hicho kilisalia dhaifu dhidi ya Real kwenye michuano miwili ya El Clasico muhula huu.

Vyombo vingi vya habari nchini Uhispania vimeripoti kwamba Koeman ambaye ni raia wa Uholanzi, atatimuliwa na Barcelona iwapo atashindwa kuongoza kikosi hicho kutia kapuni ufalme wa angalau taji moja msimu huu.

“Yasikitisha kwamba naanza kuulizwa maswali kuhusu mustakabali wangu uwanjani Camp Nou licha ya kwamba tulishuka dimbani dhidi ya Real baada ya rekodi nzuri ya kutoshindwa katika jumla ya mechi 19 mfululizo,” akasema Koeman ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Barcelona.

“Inakuwaje unapoteza mechi moja tu na tayari gumzo la kufutwa linakuwa mjadala katika vyombo vya habari? Pengine inanilazimu kuikubali hali hiyo, ila najua kwamba nina mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wangu na Barcelona. Mara nyingine presha huwa kubwa ila nyakati nyingine inabidi kukabiliana nayo,” akaongeza Koeman.

Kufikia sasa, Barcelona wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la La Liga huku pengo la alama mbili likitamalaki kati yao na viongozi wa Atletico Madrid wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone.

Mbali na kupigwa na Real kwenye michuano ya mikondo miwili ya La Liga msimu huu, Barcelona wamepoteza pia mechi muhimu dhidi ya Atletico katika mkondo wa kwanza wa La Liga. Aidha, walizidiwa maarifa na Bilbao kwenye fainali ya Super Cup na wakabanduliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Bilbao kwa upande wao wanalenga kutopoteza fainali ya pili ya Copa del Rey chini ya kipindi cha wiki mbili baada ya kuzidiwa ujanja na Real Sociedad kwenye fainali ya 2019-20 iliyoahirishwa kutoka msimu jana hadi Aprili 3, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Beckham pabaya kikosi chake kukiuka kanuni za MLS...

Man-United yadengua Granada Europa League