• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Benitez awaambia Everton wafanye juu chini ili wamsajili beki Kalidou Koulibaly wa Napoli

Benitez awaambia Everton wafanye juu chini ili wamsajili beki Kalidou Koulibaly wa Napoli

Na MASHIRIKA

KOCHA Rafa Benitez amewataka vinara wa Everton kufanya kila liwezekanalo ili kujinadia huduma za beki matata wa Napoli, Kalidou Koulibaly muhula huu.

Benitez ndiye alimsajili difenda huyo raia wa Senegal kutoka Genk ya Ubelgiji hadi Napoli mnamo 2014 kabla ya kocha huyo raia wa Uhispania kuyoyomea Real Madrid.

Ni wakati huo ambapo Koulibaly aliimarika zaidi kimchezo na kuwa miongoni mwa mabeki bora katika ulindo wa soka duniani.

Sasa akidhibiti mikoba ya Everton, Benitez anashirikiana pakubwa na mkurugenzi wa soka Marcel Brands kushawishi Napoli kumwachikilia Koulibaly, 30, kutua uwanjani Goodison Park.

Kwa mujibu wa gazeti la 90min, Napoli watakuwa radhi kumwachilia sogora huyo kuondoka kwa pamoja na kiungo Fabian Ruiz wa Uhispania ili kupunguza gharama ya matumizi ya muhula ujao wa 2021-22.4

Benitez ana kiu ya kujinasia huduma za Koulibaly ambaye gharama yake kwa sasa ni Sh5.4 bilioni ili awe kizibo cha beki raia wa Colombia, Yerry Mina, atakayeagana na Everton mwezi huu wa Julai 2021.

Ingawa rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis amekiri kwamba huenda kocha Luciano Spalletti akataka kumdumisha Koulibaly kikosini mwake, Everton wako pazuri zaidi kumtwaa sogora huyo kwa ofa ya mshahara mnono hasa baada ya kuagana na wachezaji Joshua King, Theo Walcott, Yannick Bolasie na Muhamed Besic.

Mbali na Koulibaly, Benitez anahemea pia maarifa ya Kurt Zouma wa Chelsea, Clement Lenglet wa Barcelona, Ben White wa Brighton na Takehiro Tomiyasu wa Bologna.

Everton tayari wamefichua kwamba wako pua na mdomo kukamilisha usajili wa kiungo mahiri wa Sporting CP ya Ureno, Matheus Nunes.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

ODONGO: Balaa kwa Jubilee iwapo itapigwa kumbo Kiambaa

Raia 104 wa Ethiopia watiwa mbaroni baada ya kupatikana...