• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
Benzema asaidia Real Madrid kuokota alama moja dhidi ya Atletico kwenye La Liga

Benzema asaidia Real Madrid kuokota alama moja dhidi ya Atletico kwenye La Liga

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Karim Benzema alifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia waajiri wake Real Madrid kuwalazimishia Atletico Madrid sare ya 1-1 katika gozi la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) lililowakutanisha ugani Wanda Metropolitano mnamo Jumamosi.

Kabla ya kucheka na nyavu, nyota huyo raia wa Ufaransa alishuhudia mengi ya makombora yake katika vipindi viwili vya mchezo yakidhibitiwa vilivyo na kipa Jan Oblak wa Atletico.

Luis Suarez aliwaweka wenyeji Atletico kifua mbele katika dakika ya 15 baada ya kushirikiana vilivyo na beki Kieran Trippier aliyekuwa akirejea ugani kusakata soka kwa mara ya kwanza baada ya kupigwa marufuku ya wiki 10 kwa kukiuka kanuni za mchezo wa kamari nchini Uhispania.

Trippier ambaye ni raia wa Uingereza, alipigwa marufuku ya miezi miwili na nusu pamoja na kutozwa faini ya Sh9.8 milioni na Shirikisho la Soka la Uhispania kwa hatia hiyo aliyopatikana nayo mnamo Disemba 2020.

Sare dhidi ya Real sasa inawasaza Atletico kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 59, tano zaidi kuliko nambari tatu Real ambao ni mabingwa watetezi. Barcelona wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 56 japo wao na Real wamesakata mechi moja zaidi kuliko idadi ya michuano ambayo imepigwa na Atletico ya kocha Diego Simeone.

Nusura Suarez awafungie Atletico bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila fataki yake ikapanguliwa na kipa Thibaut Courtois aliyetatizwa pia na fowadi Yannick Carrasco.

Bao ambalo Benzema aliwafungia Real lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo mvamizi raia wa Brazil, Carlos Casemiro.

MATOKEO YA LA LIGA (Machi 7, 2021):

Atletico 1-1 Real Madrid

Huesca 3-4 Celta Vigo

Sociedad 1-0 Levante

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Matumaini Lionel Messi atatia mkataba mpya Barcelona baada...

Wamiliki wa hoteli na baa Machakos waiomba serikali iondoe...