• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Chelsea wabana Liverpool licha ya kucheza kwa dakika 45 wakiwa na wanasoka 10 uwanjani Anfield

Chelsea wabana Liverpool licha ya kucheza kwa dakika 45 wakiwa na wanasoka 10 uwanjani Anfield

Na MASHIRIKA

CHELSEA walihangaisha Liverpool na kuwanyima nafasi nyingi za wazi katika kipindi cha pili kwenye mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliokamilika kwa sare ya 1-1 mnamo Agosti 28, 2021 ugani Anfield.

Hiyo ilikuwa licha ya Chelsea ya kocha Thomas Tuchel kukamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya beki Reece James kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Mechi hiyo iliyokutanisha vikosi viwili vinavyopigiwa upatu wa kutwaa ufalme wa EPL muhula huu, ulitawaliwa na hisia kali baada ya kizaazaa kushuhudiwa James alipofurushwa ugani kwa hatia ya kunawa mpira.

Tukio hilo lilishuhudia pia kipa Edouard Mendy akionyeshwa kadi ya manjano kwa utovu wa nidhamu baada ya fowadi Mohamed Salah kumfunga penalti iliyotokana na kosa la James.

Kai Havertz alifunga bao la Chelsea katika dakika ya 22 kupitia mpira wa kichwa uliomwacha hoi kipa Alisson Becker.

Mason Mount naye alipoteza nafasi murua ambayo vinginevyo ingewapa Chelsea bao la pili na kuzamisha matumaini ya Liverpool kurejea mchezoni kabla ya tukio la mwisho wa kipindi cha kwanza lililosababisha penalti.

Chelsea walikosa huduma za kiungo N’Golo Kante katika kipindi cha pili kutokana na jeraha na nafasi yake ikatwaliwa na Thiago Silva aliyeshirikiana vilivyo na Mateo Kovacic. Mendy alifanya kazi ya ziada kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na wanasoka Virgil van Dijk, Fabinho na Diogo Jota katika kipindi chote cha pili.

Uthabiti wa Chelsea waliobana sana safu yao ya ulinzi ni miongoni mwa sifa zinazowafanya mashabiki kuwapigia upatu wa kuwa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa makali yao chini ya kocha Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard mnamo Januari 2021.

Cha pekee ambacho Chelsea walikosa msimu uliopita wa 2020-21 ni fowadi wembe wa kufunga mabao kirahisi. Hata hivyo, walifaulu kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya nne na kujinyanyulia ufalme wa UEFA wakijivunia huduma za mvamizi Timo Werner aliyeshirikiana na Olivier Giroud pamoja na Tammy Abraham ambao kwa sasa wanachezea AC Milan na AS Roma mtawalia.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp waliingia ugani wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi katika mechi mbili za kwanza msimu huu dhidi ya Norwich City (3-0) na Burnley (2-0). Chelsea nao waliwapiga Crystal Palace 3-0 kabla ya kupepeta Arsenal 2-0 katika mechi mbili za kwanza.

MATOKEO YA EPL (Agosti 28, 2021):

Man-City 5-0 Arsenal

Aston Villa 1-1 Brentford

Brighton 0-2 Everton

Newcastle 2-2 Southampton

Norwich 1-2 Leicester City

West Ham 2-2 Crystal Palace

Liverpool 1-1 Chelsea

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AIK anayochezea Mkenya Eric ‘Marcelo’ Ouma...

Leicester City wazamisha chombo cha Norwich ligini